Palestina: Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya chuki wanachochea Msikiti wa Al-Aqsa uripuliwe
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i125402-palestina_walowezi_wa_kizayuni_wenye_misimamo_ya_chuki_wanachochea_msikiti_wa_al_aqsa_uripuliwe
Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa indhari kutokana na kuongezeka uchochezi unaofanywa na makundi ya walowezi wa Kizayuni wa mrengo wa kulia wanaotaka kubomolewa Msikiti wa Al-Aqsa ulioko Baitul-Muqaddas Mashariki inayokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2025-04-20T07:20:50+00:00 )
Apr 20, 2025 05:33 UTC
  • Palestina: Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya chuki wanachochea Msikiti wa  Al-Aqsa uripuliwe

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa indhari kutokana na kuongezeka uchochezi unaofanywa na makundi ya walowezi wa Kizayuni wa mrengo wa kulia wanaotaka kubomolewa Msikiti wa Al-Aqsa ulioko Baitul-Muqaddas Mashariki inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imelaani video iliyotengenezwa kwa kutumia Akili Mnemba (AI) ambayo imesambaa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ya wazayuni wenye misimamo mikali ya chuki ikiwa na anuani "Mwaka Ujao huko Jerusalem". Video hiyo inaonyesha Msikiti wa Al-Aqsa ukiripuliwa na mahala pake kujengwa kile kinachoitwa 'Hekalu la Tatu'.
 
Katika taarifa yake hiyo, wizara ya mambo ya nje ya Palestina imeielezea video hiyo kuwa ni "uchochezi ulioratibiwa unaolenga kuzidisha hujuma dhidi ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika Baitul-Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu".
 
Imesema, uongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia wa utawala wa Kizayuni wa Israel unapata uthubutu wa kuendeleza ajenda yake ya Uyahudishaji na ya kikoloni kutokana na hatua na mijibizo hafifu inayochukuliwa kimataifa kukabiliana na jinai zake za mauaji ya kimbari unayoyaendeleza dhidi ya Wapalestina, hususan wa Ukanda wa Ghaza.
 
Wakati viongozi wa utawala ghasibu wa Israel wanadai kuwa wanadumisha makubaliano ya kisheria yaliyofikiwa kuhusu Msikiti wa Al-Aqsa, Wakfu wa Kiislamu katika mji mtukufu wa Quds umeyakadhibisha vikali madai hayo.
 
Makubaliano hayo yanayorejea katika kipindi cha kabla ya 1967 yanataka Wakfu huo uwe ndiye msimamizi wa eneo la Msikiti wa Al-Aqsa na ni Waislamu pekee waruhusiwe kusali katika eneo hilo.
 
Makundi ya Kizayuni ya siasa kali za chuki za mrengo wa kulia yalikuwa yametoa mwito wa kufanyika uvamizi mkubwa dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa wakati wa sikukuu ya Pasaka ya Kiyahudi, iliyoanza Jumapili iliyopita.
 
Tangu mwaka 2003, mamlaka za utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikiwaruhusu walowezi wa Kizayuni kuvamia karibu kila siku eneo la Msikiti huo mtukufu ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.../