Hata UK, Ujerumani na Ufaransa nazo pia zalaani hatua ya Israel ya kuzuia misaada isiingizwe Ghaza
Apr 24, 2025 04:12 UTC
Ufaransa, Ujerumani na Uingereza nazo pia zimelaani hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kuzuia kikamilifu misaada ya kibinadamu isiingizwe katika Ukanda wa Ghaza, na kutoa wito wa kuanzishwa mara moja utoaji misaada bila vizuizi sambamba na juhudi mpya za kusitisha mapigano.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu zinazounda Troika ya Ulaya na ambazo ni miongoni mwa waitifaki na waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya Ghaza, wameeleza katika taarifa ya pamoja: "Israel sasa imezuia kikamilifu kuingia misaada ya kibinadamu Ghaza kwa zaidi ya siku 50," na wakaonya juu ya matokeo mabaya ya hatua hiyo kwa jamii ya Palestina.
Taarifa hiyo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa imeendelea kueleza: "bidhaa za lazima ama hazipatikani tena au zinaendelea kumalizika haraka. Raia wa Palestina - ikiwa ni pamoja na watoto milioni moja - wanakabiliwa na hatari kubwa ya kukumbwa na baa la njaa, magonjwa ya mripuko na vifo. Hili lazima likome."
Taarifa hiyo imebainisha kuwa wakati wa usitishaji vita ulioanza kutekelezwa mwezi Januari na kudumu kwa takriban miezi miwili, misaada iliweza kutolewa kwa kiwango kikubwa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali, tofauti na hali ya sasa ambayo mawaziri hao wamesema ni "isiyovumilika."
Aidha, wameonyesha kutofautiana vikali na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na waziri wa vlinzi wa utawala wa Kizayuni Yisrael Katz na mipango aliyopendekeza ya kuendelea kuwepo Israel kwa muda mrefu huko Ghaza baada ya vita.
Taarifa ya mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa imesema: "maoni ya hivi karibuni ya waziri Katz ya kuipa sura ya kisiasa misaada ya kibinadamu na mipango ya Israel kubaki Ghaza baada ya vita haikubaliki; inadhuru matarajio ya amani. Misaada ya kibinadamu haipaswi kamwe kutumika kama chombo cha kisiasa; na eneo la Palestina halipasi kupunguzwa au kuathiriwa na mabadiliko yoyote ya kidemografia. Israel inalazimika kwa mujibu wa sheria za kimataifa kuruhusu misaada ya kibinadamu ipitishwe bila kizuizi".../
Tags