Pakistan: India huenda ikaanzisha mashambulizi ndani ya saa 24 hadi 36 zijayo
(last modified Wed, 30 Apr 2025 06:35:05 GMT )
Apr 30, 2025 06:35 UTC
  • Attaullah Tarar
    Attaullah Tarar

Waziri wa Habari wa Pakistan, Attaullah Tarar amesema leo Jumatano kwamba nchi yake ina taarifa za kuaminika za kiintelijensia kwamba India inakusudia kufanya shambulizi la kijeshi dhidi ya Pakistan ndani ya masaa 24 hadi 36 yajayo, hilo likiwa tishio la hivi karibuni zaidi la vita kati ya majirani hao wawili wenye silaha za nyuklia.

Waziri huyo ameeleza - katika ujumbe wake kwenye jukwaa la kijamii la X - kwamba India itaanzisha mashambulizi ya kijeshi "kwa kutumia kisingizio cha tukio la Pahalgam (katika eneo linalozozaniwa la Kashmir)."

Attaullah Tarar ameongeza kuwa, "Uchokozi wowote utakabiliwa na jibu madhubuti na kwamba India itawajibika kikamilifu kwa matokeo yoyote mabaya katika eneo hili."

Matamshi hayo ya Waziri wa Habari wa Pakistan yanaambatana na harakati za kijeshi zinazoendelea kuongezeka kwenye mpaka wa nchi kavu wa nchi hizo mbili jirani.

Eneo la karibu na mpaka wa India na Pakistan

Mzozo wa sasa kati ya New Delhi na Islamabad umeibuka baada ya watu waliokuwa na silaha kulifyatulia risasi kundi la watalii katika eneo la kitalii la Pahalgam, lililoko takriban kilomita 90 kutoka Srinagar, mji mkuu wa majira ya joto wa Kashmir inayodhibitiwa na India, na kuua watu wasiopungua 27, Jumanne ilioyopita.

Maafisa wa serikali ya India wamelitaja tukio hilo kuwa ni shambulizi la kigaidi. India inamtuhumu jirani yake wa magharibi (Pakistani) kuwa imehusika katika shambulio dhidi ya watalii huko Kashmir.

Hata hivyo, Seneta Muhammad Ishaq Dar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, amelitaja tukio hilo kuwa ni la kusikitisha na wakati huo huo ameonya dhidi ya vitendo vyovyote vya uchochezi vinavyofanywa na jirani yake wa mashariki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema: "Kama nguvu ya nyuklia, Islamabad italipiza kisasi dhidi ya hatua yoyote ya India ili kulinda maslahi yake ya kitaifa."