Baada ya US na Israel kuishambulia kijeshi Yemen kwa pamoja, Ansarullah yasema: Tutajibu mapigo
(last modified Tue, 06 May 2025 06:15:59 GMT )
May 06, 2025 06:15 UTC
  • Baada ya US na Israel kuishambulia kijeshi Yemen kwa pamoja, Ansarullah yasema: Tutajibu mapigo

Ndege za kivita za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel usiku wa kuamkia leo zimeshambulia bandari ya Al Hudaydah magharibi mwa Yemen.

Katika mwendelezo wa hujuma na mashambulizi ya kinyama dhidi ya ardhi ya Yemen, duru za Yemen zimetangaza kuwa, usiku wa kuamkia leo, ndege za kivita za Marekani na za utawala wa Kizayuni zimeshambulia kwa pamoja bandari muhimu ya Al Hudaydah magharibi mwa Yemen. Kwa mujibu wa Pars Today, raia wasiopungua wawili wameuawa na wengine 42 wamejeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa kwa ushirikiano wa pamoja wa Marekani na wazayuni.
 
Mkuu wa Idara ya Habari ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen amelaani shambulio hilo na kueleza kuwa bila shaka Wayemen watatoa jibu dhidi ya jinai hiyo.
 
Nasreddin Amer, amesisitiza kwa kusema: "tutajibu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na hatutaondoa mzingiro wa majini na angani, bali tutaendelea na operesheni zetu za kijeshi kwa ajili ya kuunga mkono Ukanda wa Ghaza".
 
Muhammad Al-Bukhaiti, mjumbe wa Baraza la Kisiasa la harakati ya Ansarullah yeye amesema: "Operesheni za Yemen za kuitetea Ghaza zitashadidishwa hata kama zitatugharimu sana".
 
Wakati huo huo, Ismail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani hujuma ya kijeshi iliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya bandari ya Al Hudaydah na miundombinu mingine ya Yemen usiku wa kuamkia leo na kueleza kuwa shambulio hilo ni jinai ya wazi na ukiukaji mkubwa wa kanuni na sheria za kimataifa.
 
Harakati za Muqawama wa Kiislamu katika eneo za Hizbullah ya Lebanon, na Hamas na Jihadul-Islami za Palestina nazo pia zimetoa taarifa tofauti za kulaani vikali jinai iliyofanywa na utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Yemen 

Ripoti ya Kanali 12 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni inaonyesha kuwa, ndege za kivita za utawala huo ghasibu zilidondosha mabomu 48 dhidi ya watu wa Yemen katika shambulio hilo la Jumatatu usiku.

Gazeti la Kizayuni la Israel Hayom nalo pia limenukuu duru ya usalama ya utawala huo haramu na kuripoti kuwa, mbali na mashambulizi ya Marekani, ndege 30 za kivita zilishambulia bandari ya Al Hudaydah. Kwa mujibu wa chombo hicho cha habari cha Kizayuni, shambulio hilo dhidi ya Yemen lilifanyika katika awamu nane.../