Araghchi: Matamshi ya Trump juu ya Iran huko Riyadh ni ya "udanganyifu"
(last modified Thu, 15 May 2025 03:10:50 GMT )
May 15, 2025 03:10 UTC
  • Araghchi: Matamshi ya Trump juu ya Iran huko Riyadh ni ya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amepuuzilia mbali matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu ustawi na maendeleo ya Iran kuwa ya "udanganyifu" akiashiria vikwazo vya Washington dhidi ya nchi hii kwa zaidi ya miongo minne.

"Nilisikia kauli ya Rais wa Marekani jana (Jumanne) usiku; kwa masikitiko mtazamo wa udanganyifu ulitolewa," Araghchi aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa baraza la mawaziri mjini Tehran jana Jumatano.

Akizungumza mjini Riyadh Jumanne, Trump alilinganisha hali ya kiuchumi ya Iran chini ya vikwazo na ile ya Saudi Arabia ambayo alidai "imegeuza jangwa kavu kuwa shamba lenye rutuba."

Araghchi amesema kile Trump "alisema kuhusu eti uchu wa nchi za eneo wa kufurahia njia ya maendeleo na ustawi, kwa hakika, ndio njia ile ile ambayo wananchi wa Iran waliikhitari kwa mapinduzi yao na kuipeleka kuwa na nchi huru, ya kidemokrasia, huru, yenye ustawi na iliyoendelea."

"Ni Marekani ambayo imezuia maendeleo ya taifa la Iran kupitia vikwazo vyake katika kipindi cha miaka arubaini isiyo ya kawaida, kwa mashinikizo yake, na vitisho vya kijeshi na kiraia. Mwenye dhima ya matatizo ya kiuchumi ni Marekani na sera za kibeberu ambazo imeweka kwa watu wa Iran," ameongeza.

Araghchi amegusia tishio jipya la Trump la "kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu" na kuieleza Iran kuwa ni "chanzo cha ukosefu wa usalama" katika hotuba yake kwa mkutano wa uwekezaji wa Saudia na Marekani mjini Riyadh.

Ameongeza kuwa: Rais wa Marekani anapuuza jinai zote za Israel katika eneo hili na anataka kuisawiri Iran kama tishio, huu ni ujanja mtupu na upotoshaji wa vitisho. Amehoji, "Ni utawala gani ambao umeua watu 60,000 huko Gaza?"