Ghadhabu za asasi za Marekani kutokana na kushadidi jinai za Israel Ukanda wa Gaza
(last modified Wed, 21 May 2025 02:25:03 GMT )
May 21, 2025 02:25 UTC
  • Ghadhabu za asasi za Marekani kutokana na kushadidi jinai za Israel Ukanda wa Gaza

Sisitizo la utawala ghasibu wa Israel la kuendeleza vita vya kutisha vya Gaza katika mwezi wake wa ishirini na mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina, kuitumia njaa kama silaha na kuunda baa la njaa bandia huko Gaza kumepelekea kuibuka radiamali za kimataifa ikiwemo ndani ya Marekani.

Walimwengu katika maeneo mbalimbali wameghadhibishwa na hatua ya Israel ya kung’ang’ania kuendeleza vita na mauaji na hivyo kutoa wito wa kukomeshwa mara moja hali hiyo mbaya. Wakati jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza ni za wazi na zisizopingika, Marekani inazuia na kukwamisha uchunguzi wa jinai hizo unaofanywa na taasisi za kimataifa za mahakama kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Marekani pia mara kadhaa imetumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuendeleza vita huko Gaza.

Sambamba na kushadidi jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza na himaya ya Marekani na washirika wake kwa Israel, mashirika mbalimbali yameendelea kutoa indhari kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika ukanda huo. Philippe Lazzarini Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, kuzingirwa eneo hilo na utawala wa Kizayuni kunakwamisha misaada ya kibinadamu kuingia katika hilo; kwa hiyo wakazi wa eneo hilo wapo kwenye ukingo wa njaa. Shirika la UNRWA na taasisi nyingine za kimataifa mara kadhaa zimeitaka jamii ya kimataifa izuie kutokea maafa kamili ya binadamu huko Gaza na izidishe mashinikizo yake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

Maandamano ya kuunga mkoo Palestina

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani inapaswa kuhesabiwa kuwa mshirika wa moja kwa moja wa Israel katika jinai zake ambazo hazijawahi kushuhudiwa dhidi ya Wapalestina wa Gaza, kwa kuzingatia uungaji mkono wake wa kina wa kisiasa, kidiplomasia, kijeshi na kiusalama kwa Tel Aviv, pamoja na kukandamiza maandamano dhidi ya Wazayuni ndani ya Marekani.

Hata maseneta wa chama cha Democratic nchini Marekani nao wamejitokeza na kukosoa jinai za Israel huko Gaza na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ghasibu. Seneta Chris Van Hollen ameushutumu utawala wa Israel kwa kuwabakisha kwa njaa kwa makusudi raia milioni mbili wa Gaza na kusema: "Marekani inashiriki katika kukiuka sheria za kimataifa."

Kundi la wabunge 24 wa Marekani limeandika barua na kutoa wito wa kutumia njia za kidiplomasia ili kukomesha mzingiro wa Gaza.

Mashirika mbalimbali ya kiraia yameendelea kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel. Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani (CAIR) lilishutumu jamii ya kimataifa kwa kupuuza mauaji ya kimbari ya Palestina.

Sanjari na maandamano hayo, utawala haramu wa Israel umeanzisha mashambulizi mapya ya ardhini kaskazini na kusini mwa Gaza na kushadidisha operesheni zake za kijeshi.

Waziri wa vita wa Israel ametishia kupanua operesheni za kijeshi ikiwa eti hakutafikiwa makubaliano na harakati ya Hamas.

 

Marekani inaendelea kuipatia Israel silaha nzito. Si hayo tu, serikali ya Washington inazuia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuchunguza uhalifu wa Israel.

Kushadidi jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wakaazi wa Gaza na kutumia kwake ghasia na mauaji ya halaiki bila kikomo kumesababisha hata maafisa wa Marekani kushindwa kuhalalisha jinai hizo. Kwa kuzingatia mashinikizo ya maoni ya wananchi na madai ya haki za binadamu ya Wamagharibi, asasi mbalimbali za kiraia zimetaka kukomeshwa vitendo hivyo vya jinai yakiwemo mauaji ya kimbari ya Wapalestina na utumiaji njaa kama silaha dhidi ya wakazi wa Gaza.