Je, uhusiano wa serikali ya Julani na utawala wa Kizayuni unaelekea wapi?
Vyanzo vya habari vimetangaza kuwa ujumbe unaohusiana na serikali ya mpito ya Syria umefanya mazungumzo ya siri na viongozi wa utawala haramu wa Israel.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa ujumbe wa Syria uliongozwa na gavana wa zamani wa Quneitra, lakini utambulisho wa mkuu wa ujumbe wa Israel haukuwekwa wazi, ingawa ni wazi kuwa alikuwa afisa wa usalama.
Kanali ya televisheni ya Israel ya 12 pia imeripoti kuwa wiki chache zilizopita, Israel ilifanya mazungumzo ya siri na maafisa wa muundo mpya wa uongozi nchini Syria. Tovuti ya Walla News ilitangaza katika ripoti yake kuhusu suala hili na kusema, Ahmed al-Dalati, gavana wa zamani wa Quneitra na kwa sasa kamanda wa usalama wa ndani katika mkoa wa Sweida (mkoa wenye wakazi wengi wa kundi la Druze nchini Syria), ndiye anayesimamia mazungumzo hayo. Kabla ya kuangushwa serikali ya Bashar al-Assad, ndiye alikuwa ameainishwa kuwa mrithi wa kiongozi wa Ahrar al-Sham.
Habari hizi zinaonyesha kuwa uhusiano kati ya serikali ya mpito ya Syria na utawala wa Kizayuni umeingia katika awamu mpya. Serikali ya Bashar al-Assad ilianguka Desemba mwaka jana. Wakati wa uongozi wa Bashar al-Assad, Israel na Syria hazikuwa na uhusiano wa kidiplomasia, na licha ya kuwepo tofauti za kisiasa na kijiografia, aina fulani ya amani baridi ilitawala kati ya pande hizo. Utawala wa Kizayuni, ambao pia ulikuwa na nafasi muhimu katika kuupindua utawala wa Bashar al-Assad, ulikaribisha tukio hilo na unaliona kuwa moja ya matukio muhimu zaidi katika eneo la Asia Magharibi kwa maslahi yake. Siku chache kabla ya kuanguka serikali ya Bashar al-Assad, utawala huu ulitoa pigo kubwa kwa uwezo wa kijeshi wa Syria kwa kuanzisha mashambulizi makali dhidi yake.
Baada ya kuanguka Assad, utawala wa Kizayuni uliharibu miundombinu ya kijeshi ya Syria kupitia mashambulizi ya mara kwa mara, hivyo Syria kwa hakika ikawa si tishio tena kwa utawala huo unaokalia Palestina kwa mabavu. Aidha utawala wa Kizayuni pia umechukua sehemu kubwa ya ardhi ya Syria. Utawala huo umefanya mashambulizi makubwa dhidi ya Damascus katika wiki za hivi karibuni kwa kisingizio cha kuwaunga mkono Wadruze. Kuhusiana na hilo, utawala wa mpito wa Julani imeonyesha kwamba hauna uwezo wa kujibu mashambulizi ya adui na kwa hivyo umetosheka tu kwa kutoa taarifa zisizo na maana za eti kulaani mashambuli hayo.

Inaonekana kwamba moja ya sababu kuu za mazungumzo ya ujumbe wa Syria na utawala wa Kizayuni linahusiana moja kwa moja na suala hili. Ni wazi kuwa ujumbe wa Syria kupitia mazungumzo hayo umejaaribu kuushawishi utawala huo usifanye mashambulizi mapya dhidi ya nchi hiyo na kuwa tofauti zilizopo zitatuliwe kupitia mazungumzo. Katika upande mwingine, serikali ya mpito ya Syria inajaribu kufikisha ujumbe huu kwa Wazayuni kwamba katika mfumo mpya wa kisiasa, Syria si adui tena wa utawala wa Kizayuni.
Utawala wa Israel, ambao haukukaribisha mazungumzo na Syria katika miezi ya mwanzo ya kuingia madarakani Julani, sasa umegeuka na kukaribisha mazungumzo ya pande mbili. Bila shaka moja ya malengo ya Tel Aviv ni kuiburuza Syria katika mchakato wa Mkataba wa Abraham. Kwa maneno mengine, Syria, ambayo awali ilikuwa mwanachama hai na muhimu katika mhimili wa muqawama, sasa inapaswa kurekebisha uhusiano wake na utawala wa Kizayuni. Baadhi ya vyombo vya habari vya Kiibrania pia vinasisitiza kuwa licha ya kwamba mchakato huu uko katika hatua zake za awali, lakini unaweza kuwa na taathira kubwa katika muundo wa baadaye kikanda.
Aidha inaonekana kuwa kusuluhishwa mizozo iliyopo kati yake na Uturuki ni sababu nyingine ya mazungumzo ya utawala wa Israel na serikali ya Julani. Kuhusiana na hili, vyanzo vya habari katika muundo wa kijeshi wa Israel vimesema kwamba, pamoja na kuandaliwa mazingira ya kujiunga Syria katika miundo ya kikanda kama vile Mkataba wa Abraham, fursa nyingine imejitokeza kwa ajili ya kuimarisha uhusiano tata wa Tel Aviv na Ankara, kwa sababu kwa vyo vyovyote vile, Uturuki pia ni mshiriki muhimu katika mazungumzo hayo.