Jolani azidi kujikomba kwa Wazayuni, adai Syria, Israel zina maadui wa pamoja!
(last modified Sun, 01 Jun 2025 07:08:47 GMT )
Jun 01, 2025 07:08 UTC
  • Jolani azidi kujikomba kwa Wazayuni, adai Syria, Israel zina maadui wa pamoja!

Abu Mohammed al-Jolani, Mkuu wa utawala wa Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) unaoongoza nchini Syria ameliambia gazeti linalohudumia jumuiya ya Wayahudi huko Damascus kwamba, "ukweli ni kwamba, tuna maadui wa pamoja - na tunaweza kuwa na jukumu kubwa katika usalama wa kikanda."

Matamshi ya Jolani yanatilia nguvu msimamo ambao ameudumisha tangu alipotwaa madaraka baada ya kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad mnamo Disemba 2024.

Wakati huo, Jolani aliashiria mabadiliko makubwa ya kisera kwa kueleza uwazi kuelekea utawala wa Israel huku akitaja kundi la Muqawama la Hizbullah lenye makao yake makuu nchini Lebanon na Iran kuwa wapinzani wake wakuu.

"Tuko wazi kwa urafiki na kila mtu katika eneo hili - ikiwa ni pamoja na Israel. Hatuna maadui zaidi ya utawala wa Assad, Hizbullah na Iran," Jolani alisema huko nyuma katika mahojiano Disemba 9, 2024.

Licha ya mashambulizi ya anga yanayoendelea ya Israel, uvamizi wa maeneo, na wizi wa rasilimali za Syria, Jolani alisisitiza msimamo wake huo ghalati kwa jarida hilo la Kiyahudi.

Katika mahojiano yake na jarida hilo, Jolani pia alionyesha kuunga mkono kufufua kanuni za Mkataba wa Kuondoa Ushirikiano wa 1974 (Mkataba wa Dofa), akiuonyesha sio tu kama njia ya kusitisha mapigano, lakini kama msingi wa pande zote kujizuia, na ulinzi wa raia.

Mapema mwezi uliomalizika wa Mei, Jolani alithibitisha habari ya kuwepo mazungumzo "yasiyo ya moja kwa moja" kati ya utawala huo na utawala wa Israel, eti kwa lengo la kuzuia kile alichokiita mripuko usioweza kudhibitiwa wa hali ya mambo, wakati huu ambapo Tel Aviv inaendeleza uchokozi wa kijeshi usiokoma dhidi ya Syria.

Kabla ya hapo alidai kuwa Syria iko tayari kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Israel na kujiunga na Mkataba wa Abraham, lakini "kwa masharti sahihi".