Sababu za Marekani na Israel kuwapiga risasi Wapalestina kwenye safu za misaada huko Gaza
Wakandarasi wa usalama wa Marekani wanatumia risasi za moto, maguruneti, na gesi ya kuwasha dhidi ya raia katika vituo vya usambazaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Watu wa eneo hilo la Palestina ambalo limekuwa likikabiliwa na vita, mzingiro wa miaka mingi, njaa na masaibu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya sasa ya mwanadamu, hawako salama hata katika safu za kupewa msaada wa mkate. Ripoti ya uchunguzi iliyochapishwa na Associated Press (AP) kwa mara nyingine tena imefichua janga ambalo linaendelea kuwakumba watu wa Gaza chini ya kivuli cha kimya cha jamii ya kimataifa. Awali, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lilitangaza kuwa mbinu na utaratibu mpya wa Israel na Marekani kwa ajili ya kufikisha misaada kwa watu wa Gaza ni uwanja wa mauaji. AP inaripoti kuwa, wakandarasi wa usalama wa Kimarekani waliotumwa na kampuni za kibinafsi "kudhamini usalama" katika vituo vya usambazaji wa misaada huko Gaza wanatumia silaha za moto, maguruneti na gesi za kutoa machozi dhidi ya raia wa Palestina wanaokuwa kwenye safu za kupokea misaada. Wakandarasi wawili wanaoshiriki katika operesheni hiyo waliozungumza na waandishi wa habari, wametaja mienendo ya kikosi hicho cha mamluki wa Marekani na Israel kuwa ni "hatari, ya kutowajibika na ukatili," na wamefichua kuwa wanachama wengi wa kikosi hicho hawana uzoefu wa masuala ya kijeshi na waliajiriwa kupitia barua pepe siku chache kabla ya kutumwa huko Gaza. Wamefichua pia kwamba jeshi la Israel linatumia utaratibu huo wa eti usambazaji wa misaada ya kibinadamu kama chombo cha kukusanya taarifa, kujasisi watu binafsi na kudhibiti idadi ya watu wa eneo hilo.
Kwa utaratibu huo ni wazi kwamba, misaada ambayo kwa kawaida inapaswa kuwa ishara ya mshikamano wa kibinadamu imekuwa mtego wa kukusanya taarifa za kijasusi na kiusalama. Ukweli huu pia umethibitishwa na mashirika ya kimataifa. Kwa mfano tu, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema katika taarifa yake mnamo Juni 20, 2025 kwamba: "Utaratibu unaotumiwa kupeleka misaada Gaza sio njia ya kuokoa maisha ya watu, bali ni uwanja wa kifo."
Kutumia kisingizio cha misaada ya kibinadamu kwa malengo ya kijasusi kunakofanywa na utawala bandia wa Israel na Marekani huko Gaza, kama inavyothibitishwa na vyanzo vya uwanjani, sio tu kwamba kunaliondoa zoezi hilo katika safu ya masuala ya kibinadamu, lakini pia kumelifanya jukwaa la kujasusi na kufuatilia idadi ya watu wa Gaza ambao sasa wanatambuliwa kwa adui na kufuatiliwa kwa sababu tu ya kutaka kujiokoa na kuokoa familia zao kutokana na njaa. Kwa mujibu wa mamlaka rasmi ya Palestina, takriban raia 635 wameuawa wakipokea misaada tangu mchakato mpya wa usambazaji wa misaada uanzishwe na Marekani na Israel. Wengi wao ni wanawake na watoto.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kutumia wanajeshi wasio na uwezo au vikosi vya usalama katika operesheni kama hiyo sio tu kwamba ni ukiukaji wa sheria, bali pia ni ukiukwaji wa wazi wa Mikataba ya Geneva kuhusu ulinzi wa raia katika maeneo ya vita. Wakati ukiukwaji wa mkataba huu unaposababisha vifo vya mamia ya watu, kitendo hicho hutambuliwa kama uhalifu wa kivita.
Kubadilishwa misaada ya kibinadamu kuwa chombo cha ujasusi na mauaji kumewalazimisha hata watu kama Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye hutoa huduma ya mdomo tu kwa ubinadamu, kuguswa na majanga haya ya binadamu. Macron ameitaja hali hiyo kuwa "inatia aibu" na kutoa wito wa kurejeshwa taasisi za kimataifa zisizoegemea upande wowote kwenye mchakato wa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Hata hivyo hadi sasa, hakuna hatua yoyote ya vitendo iliyochukuliwa na jamii ya kimataifa hasa nchi za Magharibi zinazodai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu, isipokuwa maneno matupu. Kwa nini inakkuwa hivyo? Kwa sababu wanaouawa ni Wapalestina, na wauaji ni Wazayuni wa Israel na waungaji mkono wao wa Magharibi huko Ulaya na Marekani.
Labda swali kuu la kuulizwa hapa ni kwamba: Kama askari wa Russia wangewapiga risasi watu katika vituo vya usambazaji wa chakula nchini Ukraine, majibu ya Magharibi yangekuwaje? Je, bado nchi za Magharibi zingeendelea kutazama kwa macho tu na kukaa ukimya?
Mkanganyiko huu mkali unafichua sura halisi ya "utaratibu wa kimataifa unaodhibiti dunia ya sasa." Kanuni ya utaratibu huo ni kwamba, maisha ya binadamu yanathaminiwa kulingana na utaifa, rangi na eneo la kijiografia. Kanuni hiyo inasema kwamba, kifo cha mtoto wa Kipalestina kinapaswa kupuuzwa, na machozi ya Mpalestina hayapaswi kuonyeshwa kwenye safu za kwanza za vyombo vya habari.
Mwishoni tunasema kuwa kilichoripotiwa na Associated Press ni zaidi ya ripoti ya uwanjani; ni ripoti kuhusu hali ya maadili ya dunia ya leo. Dunia ambako chakula kinasambazwa kwa bunduki na mauaji ya wenye njaa. Gaza sio tu mwathirika wa vita bali maabara ya kuporomoka maadili ya ustaarabu wa ustaarabu wa Magharibi.