Duru ya kwanza ya mazungumzo ya kusitisha vita Kati ya Hamas, Israel yagonga mwamba
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128036-duru_ya_kwanza_ya_mazungumzo_ya_kusitisha_vita_kati_ya_hamas_israel_yagonga_mwamba
Duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano kati ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas na utawala wa Kizayuni wa Israel, iliyofanyika nchini Qatar, imemalizika bila mafanikio yoyote, kwa mujibu wa vyanzo viwili vya Palestina vinavyofahamu majadiliano hayo.
(last modified 2025-07-07T04:18:10+00:00 )
Jul 07, 2025 04:03 UTC
  • Duru ya kwanza ya mazungumzo ya kusitisha vita Kati ya Hamas, Israel yagonga mwamba

Duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano kati ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas na utawala wa Kizayuni wa Israel, iliyofanyika nchini Qatar, imemalizika bila mafanikio yoyote, kwa mujibu wa vyanzo viwili vya Palestina vinavyofahamu majadiliano hayo.

Kwa mujibu wa Iran Press, licha ya juhudi za kimataifa na duru nyingi za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, mivutano muhimu baina ya pande mbili hizo bado haijatatuliwa. Israel inapinga mapendekezo ya marekebisho yaliyowasilishwa na Hamas kabla ya kusainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, wakati ambapo harakati hiyo ya Muqawama imeonyesha nia ya kujadiliana masharti ya makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kubadilishana mateka.

Mvutano huu unaendelea huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kuwauwa kikatili makumi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kila siku, na hivyo kuzidisha idadi ya watu waliouawa katika eneo hilo lililozingirwa.

Vyanzo vya Palestina vimeripoti kuwa, "Ujumbe wa Israel haujaidhinishwa vya kutosha kufikia makubaliano na Hamas." Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema Wapatanishi wa Israel wamepwa maagizo ya wazi ya kufikia usitishaji wa mapigano kwa masharti 'yanayokubalika' kwa Israel.

Haya yanajiri licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump kudai hivi karibuni kuwa, "Kuna nafasi nzuri ya kufikia makubaliano na Hamas wiki hii. Nadhani tunakaribia makubaliano kuhusu Gaza."

Tangu Oktoba 7, 2023, idadi ya watu waliouawa shahidi katika vita vya Gaza imepindukia 57,000 huku idadi ya waliojeruhiwa ikiongezeka hadi zaidi ya watu 135,000.