Yemen yautwanga tena kombora uwanja wa ndege wa Ben Gurion, Tel Aviv
Vikosi vya Jeshi la Yemen vimeshambulia tena kwa kombora uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv katika kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza huku utawala wa kizayuni wa Israel ukiendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo uliloliwekea mzingiro.
Katika taarifa iliyotolewa leo, vikosi vya ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa vimetumia kombora la balestiki la Zulfiqar katika operesheni hiyo dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben Gurion.
Taarifa hiyo imesema, shambulio hilo la kombora "limefikia lengo lake kwa mafanikio" na kusababisha ving'ora vya anga katika miji na vitongoji zaidi ya 300 katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel.
Operesheni hiyo imewafanya mamilioni ya Wazayuni walazimike kukimbilia mafichoni na kusimamisha usafiri wa anga katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion.
Kadhalika katika taarifa yake, vikosi vya ulinzi vya Yemen vimeapa kustawisha nguvu na uwezo wake wa kijeshi na kushadidisha vita kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina.
"Operesheni hizi zitaendelea hadi uvamizi dhidi ya Ghaza utakapokoma na vizuizi kuondolewa”, imesisitiza taarifa hiyo.
Itakumbukwa kuwa, hivi majuzi, vikosi vya Yemen vilizamisha meli mbili zilizokuwa zikielekea kwenye bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel za Magic Seas na Eternity C, baada ya kukiuka marufuku ya kupita katika Bahari Nyekundu.../