Je, ushirikiano wa serikali za Magharibi na Wazayuni katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina una kiwango na mpaka?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128314-je_ushirikiano_wa_serikali_za_magharibi_na_wazayuni_katika_mauaji_ya_kimbari_ya_wapalestina_una_kiwango_na_mpaka
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza katika indhari liliyotoa hivi karibuni kwamba hali ya huduma za afya katika Ukanda wa Ghaza imefikia kiwango cha maafa.
(last modified 2025-07-14T11:55:39+00:00 )
Jul 14, 2025 11:46 UTC
  • Je, ushirikiano wa serikali za Magharibi na Wazayuni katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina una kiwango na mpaka?

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza katika indhari liliyotoa hivi karibuni kwamba hali ya huduma za afya katika Ukanda wa Ghaza imefikia kiwango cha maafa.

UNRWA imesema, imetiwa wasiwasi mkubwa na kukosekana maji ya kunywa, mrundikano wa watu katika maeneo yanayotoa hifadhi, na joto kali kupita kiasi la msimu wa kiangazi, na ikasisitiza kuwa, iwapo mzingiro lililowekewa eneo hilo utaendelea, litashuhudiwa janga la hali mbaya ya kibinadamu ambalo athari zake zitavuka mipaka ya Palestina. Shirika hilo la UN limetoa wito wa kuondolewa mara moja mzingiro na kuandaliwa mazingira ya kuwezesha kupelekwa vifaa vya huduma za afya na misaada ya kibinadamu huko Ghaza; ombi ambalo hadi sasa limepuuzwa kikamilifu na Wazayuni na kukabiliwa na kimya chenye maana maalumu cha madola ya Magharibi.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetoa takwimu za kushtusha zinazoonyesha ukubwa wa mauaji ya kimbari ya watoto huko Ghaza. Kwa mujibu wa ripoti rasmi ya shirika hilo, tangu vilipoanza vita vya kinyama vya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza mwezi Oktoba 2023, kwa wastani, watoto 27 wa Kipalestina wamekuwa wakiuliwa na jeshi la utawala huo wa kizayuni kila siku; takwimu ambazo hazijawahi kuonekana katika vita vingine vyovyote vya zama hizi katika mtazamo wa namna vilivyojikita katika kuteketeza roho za watoto wachanga. Msemaji wa UNICEF katika Ukanda wa Ghaza ameielezea hali hiyo kuwa ni "ya kikatili, isiyoweza kuhalalishwa na iliyovuka vipimo vya mantiki yoyote ya kibinadamu."

Uovu na ukatili wa Wazayuni na waungaji mkono wao wa Magharibi huko Ghaza katika kuua wanawake na watoto haukomei kwenye mashambulizi ya mabomu na makombora na mauaji ya papo hapo. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), zaidi ya watoto 5,000 wana hali ya "utapiamlo mkali," na kwa uchache watoto 66 wamefariki katika mwezi uliopita pekee kutokana na njaa, uhaba wa maziwa ya unga na ukosefu wa dawa. Katika ripoti nyingine, Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya vituo vya afya vya Ghaza havifanyi kazi tena au vimeshambuliwa moja kwa moja kwa mabomu na makombora. Takwimu hizo zinamaanisha kujiri kwa vifo vya taratibu na vya kutisha vya maelfu ya watoto, wanawake, na wakazi wa Ghaza waliopoteza makazi yao.

Mbali na majanga hayo, jeshi la utawala bandia wa Israel lingali limeuzingira kikamilifu Ukanda wa Ghaza, na hata linakabiliana kwa ukatili na Wapalestina wanaohangaika kupata misaada ya chakula. Ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imethibitisha kuwa tangu mwisho wa mwezi Mei hadi sasa, Wapalestina 798 wameuawa shahidi kwa kulengwa na wadunguaji wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel wakiwa kwenye foleni za ugawaji misaada ya kibinadamu.

Kinachotia uchungu na kuumiza zaidi kuliko majanga hayo ni upuuzaji wa makusudi unaofanywa na serikali za Magharibi. Ni serikali zinazojinasibu kuwa ndio wabeba bendera ya “haki za binadamu,” “amani ya kimataifa,” na “tunu za kidemokrasia.” Kimya cha serikali hizo si kimya cha kawaida bali ni kielelezo cha kuwa washirika katika utendaji jinai na uhalifu. Ni kimya kilichobadilika kuwa alama ya ridhaa. Serikali hizo ambazo huko nyuma zilizusha taharuki ulimwengu mzima kwa sababu ya shambulio moja la kemikali lililotokea nchini Syria, sasa hivi zinaposhuhudia mahospitali, maskuli na kambi za wakimbizi zinashambuliwa kwa makombora, hazijali kitu chochote isipokuwa “haki ya Israel ya kujilinda”. Katika mantiki mbovu na batili inayotetewa na serikali hizo, mauaji ya maelfu ya watoto ni ‘kujilinda’, lakini Muqawama na mapambano ya watu waliobakiwa na pumzi tu za kupumulia huwa ni ‘ugaidi’.

Akthari ya vyombo vya habari vya Magharibi vinachuja habari kimfumo ili kuziweka gizani fikra na maoni ya umma. Upashaji wa habari za Ghaza ama huwa ni mdogo na wa kijuujuu, au huambatana na utumiaji lugha ya kilaghai ya kuonyesha kutoegemea upande wowote. Ni kana kwamba kinachojiri ni vita kati ya majeshi mawili yenye mlingano, na si mauaji ya kinyama na kikatili yanayofanywa dhidi ya watu waliowekewa mzingiro. Kwa kuzingatia hali ya kutisha na kusikitisha ya mauaji ya kimbari ambayo haijawahi kushuhudiwa, inapasa tuseme kuwa, hakuna tena hata chembe ya dhamiri na hisia ya utu iliyosalia ndani ya nyoyo za viongozi wenye majigambo wa Magharibi. Kimya cha Magharibi si cha kutojali tu, bali ni aina mojawapo ya ushiriki hai na wa kivitendo katika jinai na uhalifu. Kama ambavyo historia imekisajili kama doa chafu litalobakia milele kimya kilichoonyeshwa mbele ya mauaji ya kimbari ya Rwanda na Srebrenica, mara hii pia itabakisha kwenye kumbukumbu ya ubinadamu majina ya serikali na taasisi zote zilizochangia mauaji ya kimbari ya Wapalestina kwa kimya chao, kwa utoaji ridhaa na kwa kushiriki kikamilifu na moja kwa moja katika mauaji hayo…/