Hamas: 'Jinamizi' la shahidi Deif linaendelea kuwaandama wahalifu wa kivita wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128320-hamas_'jinamizi'_la_shahidi_deif_linaendelea_kuwaandama_wahalifu_wa_kivita_wa_israel
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imesema urithi wa kamanda aliyeuawa shahidi Mohammad Deif utaendelea kuwaandama wahalifu wa kivita wa Israel kama "ndoto mbaya".
(last modified 2025-07-14T09:47:17+00:00 )
Jul 14, 2025 09:38 UTC
  • Hamas: 'Jinamizi' la shahidi Deif linaendelea kuwaandama wahalifu wa kivita wa Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imesema urithi wa kamanda aliyeuawa shahidi Mohammad Deif utaendelea kuwaandama wahalifu wa kivita wa Israel kama "ndoto mbaya".

Katika taarifa iliyotolewa katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza tangu kuuawa shahidi Deif, Abu Ubeida, Msemaji wa mrengo wa kijeshi wa Hamas, amesema kwamba, kamanda mkuu wa zamani wa Brigedi za Al-Qassam atasalia, kama viongozi wengine wakuu, "kinara kwa watu wote huru ulimwenguni."

"Mwaka mmoja umepita tangu kuuawa shahidi kwa kiongozi mkuu wa taifa, Kamanda Mohammad Deif, ambaye aliongoza - pamoja na ndugu zake - operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, na kutoa kwa adui Mzayuni pigo kali zaidi katika historia yake," amesema.

Haya yanajiri siku chache baada ya Brigedi za Shahid Muhammad Deif kuanzishwa rasmi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, sambamba na kutangaza utiifu wake kwa damu toharifu ya mashahidi iliyomwagwa kwenye njia takatifu ya Muqawama na ukombozi wa Palestina.

Shahid Muhammad Deif, ambaye jina lake halisi ni "Muhammad Diab Ibrahim Al-Masri," na aliyepewa lakabu ya "Abu Khaled," alizaliwa mwaka 1965 katika kambi ya wakimbizi ya Khan Yunis kusini mwa Gaza. Alikuwa kamanda mkuu wa Brigedi za Qassam, tawi la kijeshi la Hamas. Aliuawa shahidi wakati wa vita vya hivi karibuni huko Gaza pamoja na makamanda wengine kadhaa wa brigedi hizo.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaamini kuwa yeye ndiye mpangaji mkuu wa shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba, linalojulikana kwa jina la Kimbunga cha Al-Aqsa.