Ripoti: Israel inatumia droni za kiraia kuwaua watoto wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128324-ripoti_israel_inatumia_droni_za_kiraia_kuwaua_watoto_wa_gaza
Jeshi la Israel limekiri kutumia ndege zisizo na rubani za kiraia kushambulia maeneo ya Gaza, na kuua raia wa Kipalestina, aghalabu yao wakiwa watoto wadogo.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Jul 14, 2025 13:39 UTC
  • Ripoti: Israel inatumia droni za kiraia kuwaua watoto wa Gaza

Jeshi la Israel limekiri kutumia ndege zisizo na rubani za kiraia kushambulia maeneo ya Gaza, na kuua raia wa Kipalestina, aghalabu yao wakiwa watoto wadogo.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na jarida la Israel la '972 Magazine' na shirika la habari la Kizayuni la Local Call, jeshi la Israel linazitumia droni hizo zinazodaiwa kutengenezewa China kuua raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Ndege hizo zisizo na rubani zinaendeshwa na wanajeshi wa Kizayuni walio ardhini kuwaripua raia - wakiwemo watoto - ili kuwalazimisha kutoka nje ya nyumba zao au kuwazuia kurejea katika maeneo ambayo Wapalestina wamefukuzwa, vyombo hivyo viliripoti Jumapili. Vyombo hivyo viliwahoji askari na maafisa saba wa Israel katika uchungizi wao.

Kulingana na mwanajeshi mmoja aliyehojiwa na vyombo hivyo vya habari vya Kizayuni, vikosi vya Israel vilikuwa vikitumia ndege hizo zisizo na rubani, ambazo zinauzwa kibiashara kwa takriban dola 3,000, mahsusi kuwalenga watoto.

Mashambulizi ya Israel kote Gaza yamewauwa Wapalestina 47 tangu alfajiri ya leo, kwa mujibu wa duru za kimatibabu katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa, ambapo 27 waliuawa shahidi katika hujuma hizo maeneo ya kati na kusini mwa Gaza.

Vita vya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza vimeua shahidi watu zaidi ya 58,026 na kujeruhi wengine 138,520, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.