Kwa nini Wapalestina wengi wanaunga mkono misimamo ya makundi ya muqawama katika mazungumzo ya Doha?
Matokeo ya uchunguzi wa Kituo cha Uchunguzi na Utafiti wa Palestina, kwa ushirikiano na Kituo cha Kimataifa cha Sanaa, yanaonyesha kuidhinishwa na wananchi wa Palestina matakwa ya muqawama wa Palestina katika mazungumzo ya kusimamisha vita na kubadilishana wafungwa yanayoendelea huko Doha, mji mkuu wa Qatar.
Utafiti huo uliofanyika Julai 6 hadi 10, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Palestina, ikiwa ni pamoja na Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, unaonyesha kuwa 93.4% ya washiriki wanasisitiza kwamba, matakwa ya muqawama, hasa masuala yanayohusiana na misaada ya kibinadamu, mipango ya kuondoka kwa jeshi la Israel, na utatuzi wa vita ni dhamana muhimu ya kibinadamu na kimantiki na lazima izingatiwe kama sehemu muhimu ya makubaliano yoyote ya usitishaji mapigano na wavamizi na sio kulegeza kamba kuhusiana nayo.
Zaidi ya theluthi mbili ya waliohojiwa katika uchunguzi huo walisisitiza kwamba wavamizi hao watashindwa kutekeleza mipango yao ya kuwafukuza Wapalestina. Utafiti huo pia unaonyesha kuongezeka kwa uungwaji mkono wa wananchi huko Palestina kwa chaguo la muqawama.
Hapo awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilitoa taarifa na kutangaza kuwa, viongozi wa harakati hiyo wanaendelea na juhudi zao kwa umakini na uwajibikaji ili kuhakikisha duru ya sasa ya mazungumzo yanafaulu, ambayo yana lengo la kuhitimisha vita dhidi ya wananchi wa Palestina, kuhakikisha misaada ya kibinadamu inaingia kwa uhuru na salama, na kuwapunguzia watu mateso makali Gaza.
Hamas imesisitiza kwamba imechukua hatua ya kivitendo kuelekea kuendeleza mazungumzo ndani ya fremu hii. Hata hivyo, masuala ya msingi yanasalia kwenye meza ya mazungumzo, hasa kuhakikisha utolewaji wa misaada unaendelea, uondoaji kamili wa majeshi vamizi kutoka Gaza, na kutoa hakikisho la kweli la usitishaji vita wa kudumu.
Harakati hiyo imesema katika taarifa yake kwamba pamoja na kwamba mazungumzo hayo yamekabiliwa na matatizo kutokana na vizingiti na ukaidi wa utawala wa Kizayuni, Hamas inaendelea kushirikiana na wapatanishi hao kwa umakini na moyo chanya ili kuondoa vikwazo vilivyopo, kuhitimisha mateso ya wananchi wa Palestina, na kutimiza matakwa yao halali ya uhuru, usalama na maisha yenye heshima.
Hamas, kwa kutegemea uwezo wake wa kijeshi na kimkakati, imeweza kusimama kidete mbele ya jeshi la Israel. Muqawama huo wa muda mrefu, pamoja na hasara kubwa kwa Wazayuni, umewafanya wananchi wa Palestina kuamini uwezo wa makundi ya muqawama wa kukabiliana na wavamizi. Hamas pia imesisitiza mara kwa mara kwamba, mazungumzo ni mbinu ya kuchelewesha mambo tu inayotumiwa utawala wa Israel.
Wananchi wa Palestina wameshuhudia mara kwa mara utawala wa Israel ukiendelea na mashambulizi yake baada ya makubaliano ya muda ya usitishaji vita. Hatua hizi zimepelekea Wapalestina kudai dhamana ya utekelezaji katika mazungumzo mapya ya Doha.
Hamas inadai kuondolewa kabisa kwa jeshi la Israel kutoka Gaza, kurejea kwa wakimbizi, na kuachiliwa kwa mateka wa Kipalestina. Madai hayo yanawiana na matakwa jumla ya Wapalestina ya kukomesha uvamizi na kupatikana haki zao.
Watu wa Gaza pia ni watiifu kwa uongozi wa Hamas kama mwakilishi wa mapambano dhidi ya uvamizi, na hata vijana wengi zaidi wamejiunga na safu ya muqawama.
Hamas inafurahia uungwaji mkono kwa kambi ya mapambano katika eneo, ambayo yanawahakikishia watu wa Gaza kwamba kamwe hawako peke yao. Kadhalika, mabadiliko ya mitazamo ya umma duniani kwa maslahi ya Palestina na kuongezeka lawama za kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni kumeimarisha misimamo ya Hamas.
Uungaji mkono wa wananchi wa Palestina kwa misimamo ya Hamas katika mazungumzo ya usitishaji vita ni matokeo ya kuamini nguvu za muqawama, tajriba ya kihistoria ya ukiukaji wa ahadi za utawala wa Kizayuni, kuwiana na matakwa ya msingi ya muqawama wa Palestina, na uungaji mkono wa wananchi na wa kieneo kwa Hamas.
Muqawama wa Palestina ukiwa macho dhidi ya ukiukaji wa mara kwa mara wa Wazayuni kwa ahadi zao, unatilia mkazo matakwa yake ya halali katika mazungumzo ya usitishaji vita, na njia hii inaungwa mkono na Wapalestina walio wengi.