Nini lengo la utawala wa kizayuni la kuzusha mgogoro nchini Syria?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128430-nini_lengo_la_utawala_wa_kizayuni_la_kuzusha_mgogoro_nchini_syria
Utawala wa kizayuni wa Israel unaendelea na mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Syria kwa lengo la kuzusha mgogoro nchini humo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jul 17, 2025 06:42 UTC
  • Nini lengo la utawala wa kizayuni la kuzusha mgogoro nchini Syria?

Utawala wa kizayuni wa Israel unaendelea na mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Syria kwa lengo la kuzusha mgogoro nchini humo.

Ndege za kivita za Israel zilishambulia kwa mabomu maeneo yanayozunguka mji wa Izraa viungani mwa Daraa mara kadhaa. Vyombo vya habari vya Syria pia viliripoti kuwa ndege za kivita za Israel zilishambulia vituo na magari ya Wizara ya Ulinzi ya Syria mara kadhaa.

Mashambulizi haya ya jeshi la Israel yamekuja baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi na Mkuu wa Majeshi Yisrael Katz kutoa taarifa ya pamoja kuamuru jeshi vamizi la Israel kushambulia mara moja vikosi vya Syria na vifaa vilivyoingia Suwayda kusini mwa Syria.

Hii si mara ya kwanza kwa utawala wa kizayuni kushambulia ardhi ya Syria kwa madai ya usalama; baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad. Utawala unaoukalia kwa mabavu Quds uliikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Syria, ulianzisha mashambulizi makali ya anga dhidi yake kwa visingizio mbalimbali, na leo hii unatumia mashambulizi dhidi ya kabila la Druze kama kisingizio cha kuhalalisha hujuma zake za kijeshi katika ardhi ya Syria.

Mzozo kati ya makabila yanayoungwa mkono na serikali ya mpito ya Syria na makundi ya Druze katika jimbo la kusini la Suwayda umeingia katika hatua mpya kwa kutumwa wanajeshi wa wafuasi wa pande zinazozozana kutoka mikoa mingine ya Syria.

Mvutano kati ya kabila la Druze na watu wanaohusishwa na Julani sio tukio geni, na vyombo vya habari hapo awali viliripoti mapigano makali kati ya makundi yenye silaha ya Druze katika mji wa Jaramana viungani mwa Damascus na vikosi tiifu kwa Julani.

Hatua ya utawala wa kizayuni ya kuwachochea Wadruze na kutangaza uungaji mkono wake kwao dhidi ya utawala wa sasa Syria ilisababisha mvutano kati ya pande hizo mbili na kuzuka mapigano makali kati ya makundi yenye silaha ya Druze na vikosi vitiifu kwa Julani katika mji wa Jaramana.

Julani Kiongozi wa Syria

 

Katika radiamali yake kwa migogoro ya Syria, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmail Baghaei ameashiria kuendelea uchokozi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Syria, huku ukiendelea kukalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi ya Syria. Baqaei amekichukulia kitendo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua dhidi ya hatua za kivamizi za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi za eneo hili kuwa ni hatari sana na sababu ya kushadidisha kiburi cha utawala huo ghasibu.

Akisisitizia ulazima wa nchi za kieneo na ulimwengu wa Kiislamu juu ya kuzingatia kusimamisha ukiukaji na jinai za utawala wa Kizayuni yakiwemo mauaji ya kimbari ambayo hayajawahi kushuhudiwa huko Ghaza na mashambulizi yake ya mfululizo dhidi ya Syria na Lebanon, Baqaei amebainisha jukumu la jamii  ya kimataifa la kuzuia kuendelea ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kwa kushambulia mara kwa mara miundombinu ya ulinzi ya Syria (kama vile vituo vya ulinzi wa anga na utafiti), utawala wa kizayuni unalenga kuigeuza Syria kuwa nchi isiyo na uwezo wa kiulinzi ili kusiwe na kizuizi cha kukiuka anga yake.

Malengo ya utawala wa kizayuni katika kuzusha mgogoro nchini Syria ni pamoja na kuzidisha tofauti za kidini na kikabila ili kuzusha vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe, kukabiliana na uthabiti wa kisiasa na kukwamisha mchakato wa amani na pia makubaliano yoyote ya kisiasa yatakayopelekea utulivu wa ndani nchini Syria. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukitumia uungaji mkono wa Marekani hususan katika siku za hivi karibuni kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yake maovu nchini Syria.

Bashar al-Assad, Rais wa zamani wa Syria

 

Malengo ya utawala wa Kizayuni katika kuishambulia Syria ni pamoja na kupanua ardhi yake, kudhoofisha kabisa uwezo wa kiulinzi wa nchi hiyo, kutumia vibaya ukosefu wa utulivu wa ndani wa Syria, na kuweka mazingira ya kushinikiza kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Tel Aviv. Malengo hayo yamepangwa ndani ya fremu ya stratijia ya muda mrefu ya utawala wa Kizayuni ya kuongeza ushawishi wa utawala huo, Marekani na Magharibi katika eneo.

Nchi za eneo na ulimwengu wa Kiislamu kupitia uratibu na umoja zinaweza kuzima njama mbaya za mhimili wa Marekani-Uzayuni za kuzusha mgogoro katika eneo ikiwemo Syria.

Hatua za utawala wa Kizayuni katika eneo ambazo bila shaka zinatekelezwa kwa uungaji mkono wa Marekani, zimekuwa sehemu ya matukio yaliyoanza miaka kadhaa iliyopita kwa hujuma za kijeshi za Marekani na washirika wa Magharibi wa White House dhidi ya Iraq na Afghanistan, na kuweka msingi wa kuzusha mgogoro wa kiusalama na ukosefu wa utulivu katika eneo hili.