Uchunguzi: Akthari ya Waisrael wanaamini hakuna Mpalestina yeyote Ghaza 'asiye na hatia'
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika moja katika utawala wa kizayuni wa Israel umefichua kuwa idadi kubwa ya Wayahudi wa Israel wanaamini kwamba hakuna watu wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza.
aChord, kikundi cha utafiti chenye mfungamano na Chuo Kikuu cha Hebrew kilichobobea katika saikolojia ya kijamii, kimeeleza kuhusiana na matokeo ya uchunguzi wake kwamba, asilimia 76 ya umma wa Wayahudi wanakubali kwa sehemu au kikamilifu kwamba "hakuna wasio na hatia huko Ghaza", ikimaanisha kuna uhalali wa kuwaua Wapalestina wa eneo hilo.
Utafiti huo umegundua kuwa hata miongoni mwa wapiga kura wa upinzani wa Israel kwa ujumla, asilimia 47 wanaunga mkono madai hayo kikamilifu, huku miongoni mwa wapiga kura wa upinzani wa Kiyahudi, wengi wao pia wakikubaliana na madai hayo.
Mtafiti Ron Gerlitz ameyaelezea matokeo ya uchunguzi huo kuwa ni "matokeo magumu" ambayo yanaonyesha mitazamo inayoafiki mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa kizayuni wa Israel huko Ghaza.
"Matokeo haya bila shaka yanaweza kutoa mwanga juu ya idadi kubwa ya raia wa Palestina waliouawa katika vita huko Ghaza," ameandika Gerlitz kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Hisia za chuki dhidi ya Wapalestina na dhidi ya Waarabu zimekuwa zikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni ndani ya jamii ya Wazayuni, zikiwalenga Wapalestina wote katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi na Baitul Muqaddas Mashariki na vilevile Wapalestina ambao ni raia wa Israel.../