Msimamo wa karibuni wa Malaysia kuhusiana na utawala wa kizayuni na jinai unazofanya Ghaza
Malaysia imeitaka Jamii ya Kimataifa isimamishe uwanachama wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa na kuuwekea vikwazo vikali utawala huo ghasibu.
Pars Today imeripoti kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia Mohamad bin Hasan ametangaza katika mkutano na waandishi wa habari kwamba, nchi yake ilizungumzia suala la kusimamishwa uwanachama wa Israel katika Umoja wa Mataifa katika mkutano wa mwaka jana wa Baraza Kuu la umoja huo na italifuatilia tena suala hilo katika mkutano wa mwaka huu utakaofanyika mwezi ujao wa Septemba.
Bin Hasan amesisitiza: "sasa wakati umewadia wa kusimamishwa uwanachama wa Israel katika Umoja wa Mataifa; na inapasa nchi zote ziiwekee vikwazo". Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, uwekaji vikwazo unaweza kusimamisha au kupunguza upelekaji silaha kwa Israel. Kadhalika, bin Hasan amekumbusha kuwa, sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa imetoa wito kwa uwazi kabisa wa kuzuiwa utekelezaji wa mpango wa utawala wa Kizayuni wa kulikalia kwa mabavu kikamilifu na kuliangamiza eneo la Ukanda wa Ghaza.
Tarehe 29 Agosti harakati ya Hamas ilikaribisha na kupongeza wito wa Malaysia wa kusimamishwa uanachama wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa na kuwekewa vikwazo utawala huo ghasibu. Harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina ilitangaza katika taarifa kwamba, inazitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu, pamoja na nchi zote watetezi wa uhuru duniani, ziunge mkono wito huo na kutumia nyenzo zote zilizopo katika Umoja wa Mataifa kusimamisha uwanachama wa utawala huo wa kihalifu na kuuwekea vikwazo.
Kabla ya hapo, mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, wakati Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim, alipozungumzia vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na vita unavyoendeleza huko Ghaza, alitoa wito kwa walimwengu kuzidisha mashinikizo dhidi ya Israel ili "ikomeshe vitendo vyake vya uchochezi na vya utumiaji mabavu dhidi ya mataifa mengine." Anwar Ibrahim alisema: "wanaposhambulia na kuwaua wananchi wa Iran, bila shaka kutakuwa na ulipizaji kisasi. Msimamo wetu ni kuzingatiwa insafu." Waziri Mkuu wa Malaysia aliongezea kwa kusema: "huko Ghaza, mauaji yanaendelea, na yanajumuisha pia wanawake na watoto. Sasa hivi Israel inaishambulia Iran, ambayo imeamua kulipiza kisasi. Uingiliaji kati wa madola ya kigeni ikiwemo Marekani, utapelekea hali kuwa mabaya zaidi tu. Suali ni je, ikiwa Iran hairuhusiwi kujibu mapigo, kwa nini Israel inaruhusiwa kuendeleza mwenendo huo?"
Baada ya hapo pia, bila kutafuna maneno, Anwar Ibrahim alitoa hotuba ya aina yake iliyoambatana na wito wa kutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ufukuzwe katika Umoja wa Mataifa. Aliashiria jinai inazofanya Israel katika Ukanda wa Ghaza na kufanana jinai hizo na yale yaliyowahi kufanywa huko nyuma na mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apathaidi nchini Afrika Kusini na akasisitiza kwa kusema: "miaka 50 iliyopita, utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini ulifukuzwa Umoja wa Mataifa. Jinai za Israel zimevuka mipaka ya machungu na ubinadamu. Ulimwengu lazima uchukue hatua; vikwazo, kusimamishwa, na kufukuzwa."
Malaysia imetoa wito wa kusimamishwa uwanachama wa utawala wa kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa kutokana na utawala huo ghasibu kukiuka mara kwa mara sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa hususan kuhusiana na Wapalestina. Kwa kuzingatia misimamo yake ya kihistoria inayounga mkono haki za Wapalestina, serikali ya Malaysia inaamini kuwa, Israel imevuruga amani na usalama wa kimataifa kwa kupanua ujenzi haramu wa vitongoji katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, kukiuka haki za binadamu na kuendeleza mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika vita vya Ghaza. Kwa hiyo, wito huo wa Malaysia ni sehemu ya juhudi pana za kidiplomasia zinazofanywa ili kuiwajibisha Israel kwa vitendo vyake.
Malaysia imekataa kuutambua utawala wa Kizayuni na haijatambua pia unyang'anyi na ukaliaji ardhi za Palestina kwa mabavu unaoendelea kufanywa na utawala huo haramu; na inatilia mkazo kwa nguvu zote kupatikana haki na kuundwa dola huru la Palestina sambamba na kuunga mkono mapambano ya Wapalestina ya kupigania haki zao. Hii ni pamoja na kwamba, Mamlaka ya Ndani ya Palestina inao ubalozi wake katika mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur…/