Jeshi la kizayuni laporomosha jengo la ghorofa 12 linalowapa hifadhi mamia ya Wapalestina Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130458-jeshi_la_kizayuni_laporomosha_jengo_la_ghorofa_12_linalowapa_hifadhi_mamia_ya_wapalestina_ghaza
Jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel siku ya Ijumaa liliripua na kuporomosha jengo la ghorofa 12 la makazi ya raia magharibi mwa Mji wa Ghaza linalowapa hifadhi mamia ya Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao katika eneo hilo lenye msongamano wa watu na ambalo limekuwa kimbilio la makumi ya maelfu ya Wapalestina.
(last modified 2025-09-06T03:06:13+00:00 )
Sep 06, 2025 03:06 UTC
  • Jeshi la kizayuni laporomosha jengo la ghorofa 12 linalowapa hifadhi mamia ya Wapalestina Ghaza

Jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel siku ya Ijumaa liliripua na kuporomosha jengo la ghorofa 12 la makazi ya raia magharibi mwa Mji wa Ghaza linalowapa hifadhi mamia ya Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao katika eneo hilo lenye msongamano wa watu na ambalo limekuwa kimbilio la makumi ya maelfu ya Wapalestina.

Duru za Palestina zimeripoti kuwa, kabla ya kuliripua na kuliporomosha hapo jana, jeshi la utawala wa kizayuni lilishawahi kuliripua mara manne huko nyuma jengo hilo linalojulikana kama Mnara wa Mushta tangu lilipoanzisha vita vya kinyama vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza mnamo Oktoba 7, 2023, na kuharibu fleti nyingi.

Karibu na jengo hilo kuna Kambi ya Kteiba, ambayo ni moja ya kambi kubwa zaidi za Wapalestina walipoteza makazi yao inayohifadhi makumi ya maelfu ya watu.

Kinyume na madai ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel, kwamba shambulio dhidi ya jengo la Mnara wa Mushta lililenga miundomsingi ya kijeshi ya harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas, uongozi unaosimamia jengo hilo umekadhibisha vikali madai hayo na kubainisha katika taarifa kwamba: "jengo hili halina mitambo yoyote ya kijeshi au ya kiusalama na linatumika kama makazi tu ya Wapalestina waliolazimika kuhama makazi yao."

Taarifa ya uongozi wa Mnara wa Mushta imeongezea kwa kusema: "ghorofa zote zilikuwa zimefunguliwa na kuwekwa wazi, bila kuonekana silaha nyepesi au nzito".

Madai hayo ya jeshi la utawala wa kizayuni yamewashangaza na kuwashtusha pia wakazi wa eneo hilo.

Jeshi la utawala ghasibu wa Israel lilitangaza mipango ya kuyalenga na kuyabomoa majengo mengi ya ghorofa huko Ghaza katika siku zijazo, sambamba na kutoa maagizo ya kuwaamuru wakazi wa eneo hilo kuyahama maeneo yanayobolewa.

Mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa kizayuni katika Ukanda wa Ghaza yaliingia siku yake ya 700 jana Ijumaa, huku utawala huo ghasibu ukiwa umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 64,000 katika eneo hilo linalokabiliwa pia na baa la njaa.../