Hizbullah ina uwezo wa kuipiga Israel kwa makombora 7,500 angamizi
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ambayo ina viongozi wapya na kwa kiasi kikubwa viongozi wake hivi sasa ni vijana, imefanikiwa kurejesha nguvu zake na kama Israel itafanya kosa lolote la kipumbavu, basi Hizbullah ina uwezo wa kuitwanga kwa makombora 7,500 angamizi.
Hayo yameripotiwa na televisheni ya al Alam ambayo imeandika kuwa, wakati waziri wa vita wa Israel anatishia kuimaliza kabisa Hizbullah huku msemaji wa jeshi la utawala huo dhalimu, Avichay Idris, akitangaza tarehe ya mwisho ya kuwataka wananchi wa Lebanon waondoke kusini mwa nchi hiyo, sambamba na kuitishwa kikao cha baraza la vita la Israel Alkhamisi jioni (Novemba 6) ili kuandaa mpango wa kuishambulia Lebanon, wachambuzi wanasema kuwa, huenda vita baina ya Lebanon na utawala wa Kizayuni vitaanza mapema zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Televisheni ya al Alam imelinukuu jarida la Rai al-Youm linalochapishwa mjini London Uingereza likisema katika uchambuzi wa mhariri wake mkuu Abdul Bari Atwan kwamba, hali nchini Lebanon iko wazi. Hizbullah ambayo kama alivyosema Katibu Mkuu wake, Sheikh Naim Qassem, imeshajijenga upya, imepanga upya safu yake ya kijeshi, kisiasa na kiuongozi, hivi sasa ina nguvu kubwa zaidi za kujihami na ni hatari zaidi kwa utawala wa Kizayuni kuliko hahta ilivyokuwa huko nyuma.
Rai al-Youm limeandika kuwa, kwa uwezo ilio nao Hizbullah hivi sasa, ni hatari kwa Israel kuingia kwenye vita vikubwa na harakati hiyo, na hilo hata viongozi wa utawala wa Kizayuni wanalielewa vyema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vitisho vipya vya Israel dhidi ya Lebanon ni ushahidi kwamba malengo yake ya kuisambaratisha Hizbullah yamefeli.
Duru moja ya habari iliyoko karibu na Hizbullahh imesema kuwa: "Uongozi mpya wa harakati hiyo wengi wao wakiwa vijana na waliohitimu mafunzo kwenye vyuo vikuu vya nchi za Kiarabu na kimataifa, pamoja na wengine waliopata mafunzo katika vyuo vya kijeshi vya nchi kadhaa kama vile Iran, Russia na Korea Kaskazini, uko imara zaidi hivi sasa na hilo linawatia kiwewe viongozi wa utawala wa Kizayuni na Marekani.