Israel yaua watu watatu Kusini mwa Lebanon baada ya kutishia mashambulizi mapya ya kijeshi
Jeshi la Israel limewaua watu watatu katika maeneo ya kusini mwa Lebanon kupitia mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa kwa nyakati tofauti, siku chache tu baada ya kutoa onyo la kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya taifa hilo jirani.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kitaifa la Lebanon (NNA), wawili kati ya waliouawa walikuwa ndugu kutoka mji wa Shebaa, waliokuwa wakisafiri kwa gari aina ya SUV katika mteremko wa Mlima Hermon, kusini mashariki mwa nchi hiyo. Ripoti hiyo ilieleza kuwa shambulizi hilo lilisababisha gari lao kuwaka moto na hatimaye kusababisha vifo vyao.
Wizara ya Afya ya Lebanon imethibitisha idadi hiyo ya vifo, na baadaye ikaripoti kuwa mtu mwingine aliuawa na wengine wanne kujeruhiwa kufuatia shambulizi la pili lililolenga gari katika kijiji cha Baraashit.
Jeshi la Israel lilidai kuwa mashambulizi hayo yalilenga watu wanaodaiwa kuwa na uhusiano na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah. Kwa mujibu wa jeshi hilo, waathiriwa walikuwa tishio kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwaka 2024 kati ya Tel Aviv na Hizbullah, kwa lengo la kumaliza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Lebanon.
Tangu kutiwa saini makubaliano hayo, utawala wa Tel Aviv umekuwa ukitumia visingizio kama hivyo kuendeleza mashambulizi mapya dhidi ya ardhi ya Lebanon.
Awali, NNA pia iliripoti kujeruhiwa kwa watu saba kufuatia shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Israel dhidi ya gari katika mji wa Bint Jbeil, kusini mwa Lebanon.
Mauaji haya yametokea chini ya wiki moja baada ya gazeti la Maariv la Israel kunukuu jeshi la nchi hiyo likionya kuwa lipo tayari kuanzisha “operesheni ya kijeshi ya kiwango kikubwa” iwapo Hizbullah itatekeleza shambulizi lolote.
Ripoti hiyo ilisisitiza kuwa mashambulizi ya karibu kila siku yanayofanywa na Israel ni sehemu ya kile ilichokiita “vita vya uchakavu” dhidi ya Hizbullah.
Wakati huohuo, Tel Aviv imekuwa ikitumia ushawishi mkubwa wa kidiplomasia kupitia mshirika wake mkuu, Marekani, kuihimiza serikali ya Beirut kuilazimisha Hizbullah iweke chini silaha.
Hata hivyo, harakati hiyo ya mapambano imekataa vikali wito huo, ikisisitiza kuwa itaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda taifa dhidi ya uvamizi na uchokozi wa Israel, mradi tishio hilo litaendelea kuwepo.