Hizbullah yasema silaha ni muhimu kwa ulinzi wa Lebanon, haitasalimu amri kwa Marekani au Israel
-
Sheikh Naim Qassem
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kwamba wito wa Marekani na Israel wa kupokonya silaha kundi hilo la mapambano na muqawama unakusudiwa kuidhoofisha Lebanon na kuiacha ikikabiliwa na uvamizi wa kigeni.
Sheikh Naim Qassem amesema katika hotuba iliyorushwa hewani kwenye televisheni kuadhimisha Siku ya Mashahidi jana Jumanne kwamba: "Silaha za Muqawama ndio siri ya nguvu yake, na hazitasalimishwa kwa yeyote"
Amesisitiza kwamba: "vitisho na mashinikizo ya Marekani na Israel havitabadilisha msimamo wetu; tutalinda ardhi na heshima yetu na hatutasalimu amri."
"Marekani na Israel zinapaswa kukata tamaa," Sheikh Qassem aliongeza, akisisitiza kwamba Hizbullah "haitapigishwa magoti licha ya hasara na vitisho."
Ametaja wito wa kupokonywa silaha Hizbullah kuwa ni "kisingizio" cha kuanzisha uvamizi dhidi ya Lebanon, akisema, "Tunakabiliwa na tishio halisi la uwepo wetu, na ni haki yetu kufanya chochote kinachohitajika kukabiliana nalo."
Akizungumzia ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwaka jana na Israel, Sheikh Qassem amesema Israel "inakataa kuondoka katika ardhi ya Lebanon kwa sababu inataka kudhibiti mustakabali wa Lebanon."
Amsema kwamba Marekani na Israel zinaingilia kati masuala ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi ya Lebanon, akiongeza kwamba Washington inalenga "kuvunja uwezo wa Lebanon wa kupambana na kulipatia jeshi silaha kwa kiwango kinacholiwezesha kukabiliana na Muqawama", na kuiacha nchi ikiwa wazi kwa uvamizi.
"Marekani ni mradi wa uvamizi na uchokozi unaotumia Israel kama chombo cha kufikia malengo yake," amesema Katibu Mkuu wa Hizbullah.