Hamas: Kumbukumbu ya kuuawa Arafat ni kielelezo cha mwendelezo wa uhalifu wa Israel
-
Yasser Arafat
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kwamba maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya kuuawa Rais wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat, yanatukumbusha kwamba "uhalifu wa kuzingirwa uliomlenga Arafat bado unaendelea dhidi ya watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza."
Katika taarifa ya iliyotolewa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo cha Arafat, mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Hamas na mkuu wa Ofisi ya Mahusiano ya Kitaifa, Hossam Badran, amesema kwamba "kuzingirwa na kuuawa kulikomlenga rais huyo zamani wa Palestina kulikuwa sehemu ya sera ya kimfumo ya Israel ya kuwalazimisha watu wa Palestina kusalimu amri, sera ile ile inayoendelea leo katika sura tofauti."
Maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Quds yanayokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia ongezeko kubwa la ukatili wa Israel kwa miaka miwili iliyopita, sambamba na vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na Tel Aviv kwenye Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 8, 2023, ambavyo vilijumuisha kufungwa kikamifu vivuko vyote vya kuingia vijijini na mijini.
Vyanzo vya serikali ya Palestina vinasema, uhalifu huo katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Quds pekee umesababisha mauaji ya Wapalestina wasiopungua 1,069 na kujeruhiwa wengine wapatao 10,700, pamoja na kulazimika kuhama Wapalestina 50,000 na kukamatwa zaidi ya 20,500. Israel pia imeua shahidi Wapalestina wasiopungua 69,000 na kujeruhi wengiine 170,000 katika vita vya mauaji ya kimbari katikka Ukanda wa Gaza.
Badran amesema kwamba Arafat "aliuawa katika njia ya mapambano ya kupigania haki halali za kitaifa za watu wake". Amesisitiza kwamba Hamas inakumbuka roho ya Arafat na roho za mashahidi wote waliouawa katika uhalifu wa Kizayuni.
Amesisitiza kwamba "kumbukumbu ya mauaji ya Arafat inakumbusha wajibu wa umoja wa kitaifa na kuendelezwa njia ya mashahidi," na ametoa wito wa "kuanzishwa mkakati wa mapambano ya pamoja ili kukabiliana na uvamizi wa Israel na mipango yake ya kichokozi."
Kiongozi wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat alifariki dunia tarehe 11 Novemba katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa akiwa na umri wa miaka 75.
Arafat alikimbizwa Paris baada ya afya yake kuzorota akiwa katika mzingiro wa jeshi la Israel kwenye makao yake makuu mjini Ramallah, na Wapalestina wanaamini kwamba alipewa sumu.
Taasisi ya Uchambuzi wa Mionzi ya Uswisi huko Lausanne ilifichua katika uchunguzi uliotangazwa na televishenii ya Al Jazeera kwamba kulikuwapo mada ya polonium yenye mionzi katika mabaki ya mwiili wa Arafat, jambo ambalo liliimarisha tuhuma kwamba aliaga dunia kutokana na sumu hiyo ambayo hutumika katika operesheni makini sana za mauaji.