Mgogoro wa kisaikolojia miongoni mwa wanajeshi wa Israel; Wizara ya Vita ya Israel: Kujiua wanajeshi ni kielelezo cha kushindwa
Gazeti la Uingereza The Independent, limeashiria ongezeko la kiwango cha kila mwaka cha kujiua katika jeshi la Israel baada ya vita vya Gaza, na kuandika kuwa: "Zaidi ya wanajeshi 11,000 wa Israel wamekumbwa na aina mbalimbali za matatizo ya kisaikolojia baada ya vita hivyo, na takwimu kuhusu wanajeshi wanaojiua baada ya kuondoka jeshini hazijachapishwa."
Mwanzoni mwa vita vya Gaza kulichapishwa ripoti nyingi kuhusu mgogoro mkubwa wa kisaikolojia katika jeshi la Israel na matatizo makubwa ya kiakili, ikiwa ni pamoja na "tatizo la msongo wa mawazo" na matatizo mengine yanayosababisha kujiua miongoni mwa jeshi la Israel. Gazeti la Independent limeandika kuwa: Huku idadi ya wanajeshi wa Israel wanaosumbuliwa na matatizo makubwa ya afya ya akili ikiongezeka, miaka miwili baada ya vita huko Gaza, ripoti za ugonjwa wa msongo wa mawazo baada ya kiwewe, mfadhaiko na matatizo mengine ya afya ya akili miongoni mwa wanajeshi hawa zimeongezeka, na idadi ya watu wanaojiua pia inazidi kuwa kubwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takwimu za Wizara ya Vita ya Israel zinaonyesha kuwa, hadi Oktoba 7, 2023, karibu wanajeshi 11,000 wa Israel wanasumbuliwa na matatizo ya kisaikolojia. Idadi hii ni zaidi ya theluthi moja ya jumla ya wanajeshi 31,000 wa Israel waliosumbuliwa na matatizo ya kiakili katika vita vyote ambavyo Israel imehusika navyo tokea 1948, ikiwa na maana kwamba vita vya Gaza vimesababisha matatizo makubwa zaidi ya kisaikolojia kwa jeshi la Israel.
Ripoti ya Independent inaendelea kusema: Kiwango cha kujiua katika jeshi la Israel pia kimeongezeka kwa kiasi kikubwa. Katika muongo mmoja kabla ya vita vya Gaza, wastani wa idadi ya wanajeshi waliojiua katika jeshi la Israel ulikuwa wanajeshi 13 kwa mwaka, lakini tangu baada ya vita vya Gaza, idadi hiyo imeongezeka; kwa kadiri kwamba data rasmi ya jeshi la Israel zinaonyesha kuwa wanajeshi 21 walijiua mwaka jana pekee na takwimu hizi hazijumuishi wanajeshi waliojiua baada ya kuondoka jeshini. Ripoti iliyotolewa na Bunge la Israel, Knesset, mwezi uliopita ilionyesha kuwa wanajeshi wengine 279 walijaribu kujiua kati ya Januari 2024 na Julai 2025, lakini walinusurika.
Wakati huo huo, shirika la habari la Associated Press liliripoti, likiwanukuu wanajeshi kadhaa wa Israel na wanasaikolojia, kwamba wanajeshi wengi wa utawala huo ambao wamepatwa na matatizo ya kisaikolojia kutokana na vita vya Gaza wanahisi kuwa hawana lengo maishani mwao, wamepoteza mwelekeo, wanapata shida kujenga uhusiano na watu wengine, na wanazidi kukatishwa tamaa. Vyombo vya habari vya Kiebrania pia viliripoti kwamba zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Israel wanapata matibabu ya matatizo ya afya ya akili na tatizo la msongo wa mawazo.
Katika suala hili, Itamar Graf, Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkuu wa Idara ya Mipango ya Wizara ya Vita ya Israel, amesema: "Tumetoa masuluhisho kadhaa kuhusiana na suala la kujiua na tumeunda timu za wataalamu wa tiba ya akili na saikolojia ili kufuatilia visa vya wanajeshi wanaojiua, lakini kwa bahati mbaya, kuna visa vingi vya kujiua miongoni mwa wanajeshi wa Israel na tunashuhudia ongezeko la jambo hili; kila kisa cha kujiua ni kielelezo cha kushindwa kwetu."
Profesa Hagai Hermes, mtaalamu wa magonjwa ya akili na mwanzilishi wa chama cha "For Life", pia anasema: "Takwimu zinazotolewa kuhusu kujiua katika jeshi la Israel ni tone dogo tu la mlima wa barafu, na kati ya wanajeshi 500 na 700 hujiua kila mwaka; takwimu hizi zimefichwa na hazitolewi kwa vyombo vya habari." Vilevile, Profesa Yossi Levi Belaz, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Vitendo vya Kujiua katika Chuo Kikuu cha Rupin, ameonya kuhusu suala hili akisema, kwa kuzingatia takwimu za kujiua katika jeshi la Israel, inaonekana kwamba wimbi kubwa la kujiua miongoni mwa wanajeshi linakuja kwa kasi.