Vitisho vya mzayuni vyaifanya serikali ya Al-Jolani ifute maadhimisho ya Kimbunga cha Al-Aqsa
Duru za habari zimeripoti kuwa kongamano la Operesheni ya Muqawama wa Palestina dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel ya Kimbunga cha Al-Aqsa, lililokuwa limepangwa kufanyika katika mji wa Aleppo nchini Syria limefutwa baada ya mwandishi mmoja wa habari wa Kizayuni kutoa vitisho kwa kiongozi wa mpito wa nchi hiyo, Al-Jolani na serikali yake.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Syria, mwandishi wa habari wa Kizayuni Edi Cohen aliweka kwenye mtandao wa kijamii X, andiko la onyo akimhutubu Al-Jolani na serikali yake akisema: "muna muda wa hadi saa sita mchana leo (Ijumaa) kufuta mkutano huu na Waziri wa Utamaduni wa Syria kuomba msamaha kwa hatua hii".
Katika andiko lake hilo, Cohen vilevile alitoa wito kwa Al-Jolani wa kumtaka amwachishe kazi Muhammad Yassin Saleh ambaye ni Waziri wa Utamaduni wa Serikali ya Mpito ya Syria.
Kufuatia kitisho hicho, kongamano hilo la kuadhimisha Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa katika mji wa Aleppo lilifutwa kwa kisingizio cha kufanyika sherehe nyingine kwenye ukumbi uliokuwa umepangwa kwa ajili ya hafla hiyo.
Kurugenzi Kuu ya Utamaduni ya Aleppo hapo awali ilikuwa imetangaza wakati wa kufanyika sherehe hiyo kuwa ni saa 11 jioni leo (Ijumaa) na kutoa wito kwa wananchi kushiriki kwa wingi.
Hafla hiyo ilikuwa imeandaliwa kwa ushirikiano na vikundi vya sanaa vya Palestina na Kurugenzi Kuu ya Utamaduni ya Aleppo.../