HAMAS: Kwa msaada wa Iran, Muqawama una nguvu zaidi hivi sasa katika kukabiliana na adui Mzayuni
Mmoja wa makamanda wa Harakati ya Muqawama wa Ghaza amesema kuwa: Maadui walitaka kusambaratisha Muqawama kupitia vikwazo na mashinikizo, lakini kwa msaada wa Iran, Muqawama una nguvu zaidi hivi sasa za kupambana na adui Mzayuni kuliko hata ilivyokuwa huko nyuma.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars kutoka Yasuj, Hisham Salem ambaye ni mmoja wa makamanda wa HAMAS amesema hayo katika mkutano wa 16 wa wajumbe wa kidini na kamati ya kuwakumbuka mashahidi wa jihadi uliofanyika kwenye Husseiniyah ya Sarallah mjini Yasuj, kusini magharibi mwa Iran.
Huku akilishukuru taifa la Iran kwa kuiimarisha kambi ya Muqawama, amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na mataifa kama ya Lebanon, Palestina, Iraq na Yemen, yameunda umoja imara dhidi ya utawala vamizi wa Kizayuni.
Ameongeza kuwa: Mshikamano huo ni urithi wa chuo cha Imam Khomeini (MA) na ni mwendelezo wa nguvu za Muqawama wakati wa uongozi wa busara sana wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Amesema: Taifa la Iran ndiyo nguzo kuu ya mapambano dhidi ya maadui wa Uislamu na ndiye kiongozi wa kambi ya Muqawama katika eneo hili lote.
Kamanda huyo wa Muqawama wa huko Ghaza ameendelea kusema kuwa: Leo, nguvu na mamlaka ya kambi ya Muqawama katika nchi za Lebanon, Palestina, Iraq na Yemen ni matokeo ya uungaji mkono na misimamo ile ile ya kishujaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Muqawama wa taifa la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani umekuwa ni kigezo kinachofuatwa na mataifa huru ya dunia.
Akigusia hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza, Hisham Salem amesema: Zaidi ya asilimia 80 ya watu wa Ghaza wanaishi katika hali ngumu ya vita na wananyimwa mahitaji ya msingi mno kama vile maji, chakula, dawa na maziwa ya unga kiasi kwamba bei ya kifurushi cha maziwa ya unga imefikia zaidi ya dola 80 na watoto wengi wanakufa kutokana na kuzingirwa na ukosefu wa dawa.
Salem amemalizia kwa kusema: Watu wa Ghaza leo hii wako katika hali sawa na siku ya Ashura ya Hussein ibn Ali (AS). Amesema: Kama Ahl al-Bayt walivyokandamizwa huko Karbala, taifa la Palestina pia leo hii limesimama kwenye njia ya haki na uhuru chini ya mashambulizi ya adui.