Shida na umasikini; urithi ambao utawala wa kizayuni umewaachia watu wake kutokana na vita vya Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134140-shida_na_umasikini_urithi_ambao_utawala_wa_kizayuni_umewaachia_watu_wake_kutokana_na_vita_vya_ghaza
Matokeo ya uchunguzi uliofanywa na shirika moja la Kizayuni la utoaji huduma na misaada ya kibinadamu yanaonyesha kuwa, vita vya Ghaza vimewatumbukiza Wazayuni wengi zaidi kwenye lindi la umasikini; na zaidi ya robo ya familia, sasa zinakabiliwa na uhaba wa chakula.
(last modified 2025-12-10T04:24:14+00:00 )
Dec 10, 2025 04:24 UTC
  • Shida na umasikini; urithi ambao utawala wa kizayuni umewaachia watu wake kutokana na vita vya Ghaza

Matokeo ya uchunguzi uliofanywa na shirika moja la Kizayuni la utoaji huduma na misaada ya kibinadamu yanaonyesha kuwa, vita vya Ghaza vimewatumbukiza Wazayuni wengi zaidi kwenye lindi la umasikini; na zaidi ya robo ya familia, sasa zinakabiliwa na uhaba wa chakula.

Shirika la Latet, ambalo lilianzishwa mwaka 1996 kwa madhumuni ya kupunguza kiwango cha umasikini na uhaba wa chakula katika jamii ya wazayuni, limetahadharisha katika ripoti liliyotoa hivi karibuni kwamba zaidi ya robo ya familia katika maeneo wanayoishi wazayuni hao, hivi sasa zinakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na athari hasi za kiuchumi na kijamii za vita vya miaka miwili huko Ghaza.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, Latet imefichua kuwa, karibu asilimia 27 ya familia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel, zikiwa ni takribani kaya 867,256 zinakabiliwa na uhaba wa chakula. Imeelezwa katika ripoti hiyo kwamba, uhaba huo wa chakula unawakabili hata watoto pia.

Latet imeielezea hali hiyo kuwa ni mgogoro unaoshadidi katika maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu.

Ombaomba Israel

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna "tabaka jipya la mafakiri" limejitokeza katika jamii ya wazayuni, na kwamba robo ya wanaopokea msaada wa chakula ni wale ambao wamepatwa na umaskini ndani ya kipindi cha miaka miwili tu ya sasa, yaani tangu vilipoanza vita vya Ghaza.

Likinukuu ripoti ya uchunguzi huo uliofanywa na shirika la Latet, gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limeripoti kuwa, mshtuko wa kiuchumi wa Oktoba 7 umezidisha hali ya ukata iliyopo na kutumbukiza maelfu ya familia kwenye lindi la umasikini. Wamiliki wa biashara ndogondogo na watu wanaopata mishahara kwa kuwepo kazini muda wote, ambao kabla ya vita vya Ghaza walikuwa wanaweza kujikimu kimaisha, sasa wanakabiliwa na mzigo wa kupanda kwa bei za chakula na gharama za nyumba pamoja na ongezeko la madeni.

Vita vya Ghaza vimepelekea kuporomoka uchumi wa utawala wa kizayuni wa Israel; na mashinikizo ya kifedha yaliyotokana na gharama za vita, kupanda kwa bei za bidhaa na kupungua kwa kipato vimewasukuma na kuwatumbukiza mamilioni ya watu kwenye lindi la umasikini na uhaba wa chakula.

Hali ngumu ya kiuchumi inayoendelea kushuhudiwa katika jamii ya wazayuni imezidisha pia mgogoro wa matatizo kisaikolojia na kijamii, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wanaopokea misaada ya kijamii wameeleza kwamba hali zao kisaikolojia ni mbaya, na watoto wengi wamekuwa wakikosa fursa za kielimu na kijamii.

Netanyahu

 

Baraza la mawaziri la Netanyahu limeshindwa kupata suluhisho athirifu kwa hali mbaya ya kiuchumi inaoukabili utawala wa kizayuni. Sehemu kubwa ya rasilimali za fedha zimetengwa kwa ajili ya vita, na programu za utoaji misaada zimesimamishwa. Vita vya Ghaza havijautwisha utawala wa kizayuni mzigo mzito wa gharama za kijeshi tu, lakini vimeufanya uchumi wake pia udorore na kuongeza makali kwa umasikini wa kimuundo. Mashinikizo ya madeni kwa familia yanaonyesha kuwa, hali mbaya ya kiuchumi na kijamii ndani ya jamii ya Wazayuni imefikia kiwango ambacho hata tabaka la kati, sasa halimudu kuendelea kuishi maisha ya kawaida.

Ukweli ni kuwa, vita vya Ghaza havijawa na athari kubwa na hasi za kibinadamu na kiusalama pekee, lakini pia vimeathiri vibaya mno uchumi wa utawala wa Kizayuni. Mgogoro wa kiuchumi unaoshuhudiwa Israel ni wa kimuundo na wa pande kadhaa ambao umetokana na vita vya Ghaza na uzembe wa kiutendaji wa Netanyahu. Mgogoro huo umeufanya utawala wa kizayuni uzidi kupoteza uhalali wa kisiasa na kuuweka hatarini zaidi mustakabali wake…/