Katibu Mkuu wa UN alaani vikali hatua ya Israel ya kubomoa majengo ya UNRWA Quds Mashariki
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kitendo cha vikosi vya utawala wa kizayuni wa Israel cha kubomoa majengo yaliyomo ndani ya eneo la makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) katika mji wa Baitul Muqaddas Mashariki unaokaliwa kwa mabavu.
"Katibu Mkuu analaani vikali kabisa vitendo vya mamlaka ya Israel cha kubomoa majengo ya UNRWA ya eneo la Sheikh Jarrah," ameeleza msemaji wa Guterres, Farhan Haq wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya UN mjini New York.
Huku akiashiria kinga ya kisheria na ya kutofanyiwa ukiukaji wa aina yoyote majengo ya Umoja wa Mataifa, Haq amesema: "kwa mtazamo wa Katibu Mkuu vitendo vinavyoendelea kufanywa kwa kasi dhidi ya UNRWA, ambavyo haviendani na majukumu ya wazi iliyonayo Israel chini ya sheria za kimataifa, ukiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Upendeleo na Kinga ulizonazo Umoja wa Mataifa havikubaliki hata kidogo."
"Katibu Mkuu anaihimiza serikali ya Israel isitishe mara moja ubomoaji katika eneo la UNRWA la Sheikh Jarrah, na kuliweka kwenye hali yake ya asili jengo hilo na majengo mengine ya UNRWA na kuyarejesha bila kuchelewa kwa Umoja wa Mataifa," ameongezea kueleza Haq.
Mwezi uliopita, Bunge la Israel, Knesset lilipitisha sheria ya kukata umeme na usambazaji wa maji kwa majengo ya UNRWA yaliyoko Baitul-Muqaddas Mashariki.
Huko nyuma pia, Israeli ilichukua hatua kama hizo dhidi ya UNRWA. Mnamo mwaka 2024, Knesset ilipitisha sheria ya kupiga marufuku shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa huko Israel, ikitoa madai kwamba baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walihusika katika matukio ya Oktoba 7, 2023, madai ambayo shirika hilo limeyakanusha. Umoja wa Mataifa umesema UNRWA inafungamana na msingi wa kutoegemea upande wowote.../