Trump atishia kuikatia misaada Iraq endapo Nouri al-Maliki atakuwa Waziri Mkuu
Rais wa Marekani Donald Trump amedai katika ujumbe unaoakisi uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Iraq kwamba Nouri al-Maliki hapasi kuwa waziri mkuu, kwa sababu kama atachaguliwa kushika wadhifa huo, Marekani haitatoa tena misaada kwa nchi hiyo.
Trump ameandika katika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social akisema: "nimesikia kwamba nchi kubwa ya Iraq inaweza ikafanya chaguo baya kwa kumchagua tena Nouri al-Maliki kuwa waziri mkuu wa nchi hii".
Pasi na kuashiria athari hasi na mbaya za hatua ya Marekani ya kuingilia masuala ya ndani ya Iraq kwa uchumi wa nchi hiyo, rais huyo wa Marekani amedai pia kwamba, mara ya mwisho al-Maliki alipokuwa madarakani nchini Iraq, nchi hiyo ilitumbukia kwenye umasikini na machafuko, na kuongezea kwa kusema: "hatupaswi kuruhusu hili litokee tena."
Trump amehitimisha ujumbe wake huo kwenye mtandao wa Truth Social kwa kutishia kwamba, ikiwa al-Maliki atakuwa tena waziri mkuu wa Iraq, Marekani haitaisaidia nchi hiyo, akidai: "katika hali hiyo, Iraq haitakuwa na nafasi ya kupata mafanikio, na kuwa na ustawi au uhuru."
Vyombo vya habari vya Iraq viliripoti Jumamosi usiku kwamba, Mfumo wa Uratibu, unaoundwa na mirengo ya kisiasa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq umetoa taarifa ukieleza kwamba umemchagua Nouri al-Maliki kuwa mgombea wa uwaziri mkuu wa nchi hiyo kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 11 Novemba mwaka jana.../