Njama ya 'genge la Netanyahu' ya kushambulia Masjidul Aqsa kwa makombora yatibuka
Wizara ya Intelijensia ya Iran imefichua njama chafu iliyokuwa ikipikwa na genge la Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu ya kushambulia kwa makombora Msikiti wa al-Aqsa ili kuibua fitna katika ulimwengu wa Kiislamu.
Afisa mmoja wa wizara hiyo amenukuliwa na shirika la habari la ISNA akisema kuwa, utawala haramu wa Israel unapanga kushambulia Masjidul Aqsa kwa makombora ukitarajiwa kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italaumiwa na kubebeshwa dhima ya shambulio hilo.
Ameeleza bayana kuwa, lengo la Wazayuni kupika majungu hayo ni kuibua migawanyiko na fitna kati ya ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu kwa upande mmoja, dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Tayari utawala wa Kizayuni umeanza kuwahamisha Wayahudi wanaoshi karibu na Masjidul Aqsa, huku ukiendeleza mashambulizi dhidi ya Iran kwa ushirikiano na Marekani.
Afisa huyo wa Wizara ya Intelijensia ya Iran amewataka Waislamu kuwa macho mkabala wa njama zinazopikwa na Wazayuni, ikiwemo ya kushambulia Msikiti wa Aqsa, siku chache kabla ya maadhimisho ya Siku ya Quds.
Mamilioni ya watu kote duniani wamekuwa wakishiriki kila mwaka katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, kuonyesha mshikamano na Palestina, na kulaani ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hasa katika Ukanda wa Gaza.
Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilitangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, kwa shabaha ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kupigania ukombozi wa Quds Tukufu.
Haya yanajiri huku jeshi la Israel kikiendelea kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, hasa katika vituo vya ukaguzi vinavyoelekea katika mji wa Quds (Jerusalem), sanjari na kuimarisha vizuizi dhidi ya Wapalestina wanaotaka kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa kwa ajili ya Swala na ibada nyinginezo katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.