Ansarullah Yemen: Lobi ya Wazayuni imezuia makubaliano kati ya Marekani na Iran
Mjumbe wa Idara ya Siasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa lobi ya utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Marekani imezuia kufikiwa makubaliano katika mazungumzo kati ya Marekani na Iran.
Muhammad al-Far’ah, mjumbe wa Idara ya Siasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen, ameandika katika ukurasa wake binafsi kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Ni jambo la kawaida kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran yameshindikana, kwa sababu rahisi nayo ni kwamba, adui Mzayuni, na nyuma yake, lobi ya utawala wa Kizayuni hawataki utulivu duniani wala kusimamishwa vita katika eneo hili.”
Amesisitiza kuwa, hali ya Marekani wala ya washirika wake wa Kiarabu si muhimu kwa lobi ya utawala wa Israel, kama ambavyo pia hawajali mgogoro wa Ulaya, na hawaoneshi hisia yoyote kwa dunia inayoteseka kutokana na mfumuko wa bei na mgogoro wa nishati.
Muhammad al-Far’ah ameongeza: “Wayahudi wa Kizayuni hawataki dunia iwe na utulivu, na kila mtu ameona jinsi Israel ilivyoshambulia Lebanon ili kuvuruga mazungumzo na kuendeleza uvamizi wake. Lakini bila shaka watashindwa, na hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu."
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa harakati ya Ansarullah nchini Yemen amesema: Hata hivyo, Wazungu wanapaswa kujua ni nani chanzo cha migogoro hii yote, na Wamarekani wanapaswa kuelewa kuwa kaulimbiu halisi ya Trump ni ‘Israel Kwanza’, siyo ‘America First’.”