Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka: Hali ya maisha huko Gaza ni ya kutisha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i137842-shirika_la_madaktari_wasio_na_mipaka_hali_ya_maisha_huko_gaza_ni_ya_kutisha
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetoa onyo kuhusu kuendelea na kuongezeka kwa mashambulizi ya kikatili na udhibiti wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-04-13T12:08:32+00:00 )
Apr 13, 2026 11:59 UTC
  • Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka: Hali ya maisha huko Gaza ni ya kutisha

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetoa onyo kuhusu kuendelea na kuongezeka kwa mashambulizi ya kikatili na udhibiti wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Shirika hilo la kimataifa limefichua katika taarifa yake kwamba kile kilichotekelezwa kama “kusitisha mapigano” tangu Oktoba mwaka jana hakijafanikiwa kabisa katika kumaliza mateso ya watu wa Ukanda Gaza. Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo, tangu wakati huo kwa uchache watu 733 wameuawa na wengine 1,913 wamejeruhiwa katika eneo hilo la Palestina.

Timu za kitabibu za MSF zimeripoti kuwa zimefanya zaidi ya matibabu 40,000 ya majeraha yanayotokana na ukatili mkubwa (ikiwa ni pamoja na kupigwa risasi moja kwa moja na milipuko ya mabomu). Pia limesisitizwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaotembelea kliniki za shirika hilo katika mji wa Gaza wana majeraha yaliyosababishwa moja kwa moja na mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

Claire San Filippo, mkuu wa dharura wa shirika hilo, amesema: “Wavamizi wanataka kuangamiza kabisa hali ya maisha huko Gaza kwa kuweka vikwazo vya makusudi katika kuingiza misaada na kufuta usajili wa mashirika 37 ya kimataifa ya msaada.”

Ameongeza kuwa shirika hilo tangu mwanzoni mwa mwaka huu (2026) halijaruhusiwa hata kuingiza shehena moja ya vifaa vya kitabibu katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mfumo wa afya wa Gaza unakabiliwa na ukandamizaji wa kimakusudi na uliopangwa.

Kwa sasa zaidi ya wagonjwa 18,500, wakiwemo watoto 4,000, wanahitaji kuhamishwa mara moja kwa ajili ya matibabu, lakini maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanazuia kuondoka kwao. Aidha, kutokana na kuhamishwa kwa lazima asilimia 90 ya wakazi wa eneo hilo na msongamano mkubwa, magonjwa ya ngozi, tumbo na mfumo wa upumuaji yamesambaa sana huko Gaza.

Katika maeneo ya operesheni, Madaktari Wasio na Mipaka wamefichua kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni limegawanya Ukanda wa Gaza kwa kuunda eneo linaloitwa mstari wa manjano, na kuwalazimisha Wapalestina kubaki katika asilimia 42 tu ya maeneo yaliyoharibiwa. Maeneo yanayozunguka mstari huo yamegeuzwa kuwa eneo la mauaji, ambalo mara kwa mara liko chini ya mashambulizi makali ya anga, mizinga na meli za kivita za Israel.

Mwishoni, shirika la MSF limeiomba jumii ya kimataifa na nchi za Kiarabu kuweka mashinikizo ya kisiasa ili kulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel, kama dola vamizi na linalokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, kulinda raia, kurejesha mazingira ya maisha ya kibinadamu na kuruhusu kuingia misaada ya kitabibu na kibinadamu bila masharti yoyote.