Kiongozi Muadhamu atoa msamaha kwa wafungwa 139 waliohukumiwa adhabu ya kifo Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i139136-kiongozi_muadhamu_atoa_msamaha_kwa_wafungwa_139_waliohukumiwa_adhabu_ya_kifo_iran
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, ameidhinisha pendekezo la kubadilisha hukumu za wafungwa 139 waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama mbalimbali nchini.
(last modified 2026-06-14T12:05:06+00:00 )
Jun 14, 2026 12:03 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei
    Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, ameidhinisha pendekezo la kubadilisha hukumu za wafungwa 139 waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama mbalimbali nchini.

Msamaha huo umetolewa kufuatia ombi la Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini, Gholam Hossein Mohseni‑Ejei.

Msemaji wa Mahakama ya Iran, Ali Asghar Jahangir, amesema kuwa Ayatullah Khamenei ametoa uamuzi huo kwa kuzingatia misingi ya huruma katika Uislamu. Amesisitiza kuwa hatua hiyo imechukuliwa katika wakati ambapo nchi nyingi duniani hukataa kutoa msamaha wa aina hiyo wakati wa vita au nyakati za misukosuko.

Aidha amebainisha kuwa wafungwa waliohukumiwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa pamoja na wale waliotuhumiwa kuhusika katika ghasia za Januari zilizoungwa mkono na tawala za kigeni, pamoja na vitendo vya hujuma, hawakujumuishwa katika orodha ya waliopata msamaha.

Kwa mujibu wa Ibara ya 110 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kiongozi ana mamlaka ya kusamehe au kupunguza adhabu za wafungwa baada ya kupokea pendekezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mahakama.

Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu baadhi ya makundi ya wahalifu, wakiwemo waliopatikana na hatia ya kushiriki katika mapambano ya silaha dhidi ya nchi, biashara ya dawa za kulevya kwa silaha au kwa mtandao uliopangwa, uporaji wa kutumia silaha, usafirishaji haramu wa silaha, utekaji nyara, rushwa, na ubadhirifu wa mali.