Kwa nini Netanyahu atasajiliwa katika historia kama waziri mkuu mbaya zaidi wa utawala wa Kizayuni?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140274-kwa_nini_netanyahu_atasajiliwa_katika_historia_kama_waziri_mkuu_mbaya_zaidi_wa_utawala_wa_kizayuni
Gazeti la Haaretz limeandika: Netanyahu atasajiliwa katika historia kama waziri mkuu mbaya zaidi wa utawala wa Kizayuni. Gazeti hilo limechapisha ripoti inayokosoa vikali utendaji wa Benjamin Netanyahu, likisisitiza kuwa atakumbukwa kama Waziri Mkuu mbaya zaidi wa utawala wa Kizayuni na kwamba madhara ya kiusalama na kiuchumi ya vita alivyovisababisha yataukabili utawala wa Israel kwa miaka mingi ijayo.
(last modified 2026-07-30T06:58:57+00:00 )
Jul 30, 2026 06:54 UTC
  • Kwa nini Netanyahu atasajiliwa katika historia kama waziri mkuu mbaya zaidi wa utawala wa Kizayuni?

Gazeti la Haaretz limeandika: Netanyahu atasajiliwa katika historia kama waziri mkuu mbaya zaidi wa utawala wa Kizayuni. Gazeti hilo limechapisha ripoti inayokosoa vikali utendaji wa Benjamin Netanyahu, likisisitiza kuwa atakumbukwa kama Waziri Mkuu mbaya zaidi wa utawala wa Kizayuni na kwamba madhara ya kiusalama na kiuchumi ya vita alivyovisababisha yataukabili utawala wa Israel kwa miaka mingi ijayo.

Kushindwa kwa Netanyahu hakutapimwa tu kwa matukio ya tarehe 7 Oktoba 2023 (Operesheni ya Kimbinga cha Al-Aqsa) bali pia kwa gharama kubwa ya kiuchumi iliyotokana na tukio hilo. Taswira ambayo Netanyahu alijijengea kama "mtu wa amani" katika kipindi kirefu cha shughuli zake za kisiasa ilisambaratishwa na matukio ya tarehe 7 Oktoba. Gazeti la Haaretz limebainisha kuwa tangu tarehe 7 Oktoba, walowezi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wamepitia mojawapo ya vipindi hatari zaidi vya vitisho vya usalama katika historia ya utawala huo, na kwa hakika, hali mbaya zaidi katika kipindi cha vizazi viwili.

Netanyahu aliwaahidi mara kwa mara Wazayuni kwamba "angeiangamiza kabisa Hamas" na "kuwaletea ushindi wa kweli," lakini Haaretz linasisitiza kuwa ahadi hizo hazijatekelezwa. Hamas si tu haijapokonywa silaha, bali vita vya Gaza vimegeuka kuwa kinamasi kigumu na chenye kuchosha ambacho hakikuleta ushindi wa kijeshi wala usalama wa kudumu. Kwa maneno mengine, kushindwa Netanyahu hakukomei kwenye tukio lenyewe la tarehe 7 Oktoba, bali kunaenea hadi kwenye madhara yake ya kiusalama na kiuchumi.

isitoshe, gazeti la Haaretz linataja suala la Iran, kufuatia tukio la tarehe 7 Oktoba, kama kushindwa kukubwa kwa pili katika kipindi cha uongozi wa Netanyahu. Kwa mujibu wa gazeti hilo, suala la Iran linaibuka kama janga kubwa la pili katika kipindi kirefu cha uongozi wa Netanyahu, likifuatia hujuma kali iliyofanywa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023. Netanyahu, ambaye amekuwa akiita mapambano dhidi ya Iran kuwa "mradi wa maisha yake," amekumbwa na kushindwa kimkakati katika uwanja huu pia. Kwa hakika, shambulio dhidi ya Iran si tu limeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa, bali pia limeusukuma utawala wa Kizayuni kuelekea "kushindwa kimkakati" na kudhoofisha uungaji mkono wa Marekani. Katika uchambuzi mwingine, gazeti la Haaretz linasisitiza kuwa vita vya Netanyahu dhidi ya Iran ndiko kushindwa kukubwa zaidi katika maisha yake, tena kubaya zaidi hata kuliko tukio la tarehe 7 Oktoba.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, vita vya kichokozi vya Israel huko Gaza, Lebanon, na Iran vimeshindwa kufikia malengo ambayo Netanyahu aliyaweka, ambapo Hamas bado ina silaha huko Gaza, Hizbullah haijashindwa kijeshi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado imesimama imara. Kiuhalisia, kushindwa Netanyahu si katika uwanja wa kijeshi pekee. Mambo mengine kama vile ongezeko kubwa lisilo na mfano wake katika bajeti ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni, kupanda kodi, kupunguzwa kwa huduma za umma, na kuongezeka kwa deni la taifa, yote hayo yatakuwa na matokeo ya muda mrefu katika uchumi wa utawala huo na hali ya maisha ya Wazayuni. Kwa maneno mengine, Wazayuni wanaoishi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu watalipa gharama kubwa kutokana na makosa makubwa ya kimkakati ya Netanyahu.

Hivyo, kilichomfanya Netanyahu kuwa waziri mkuu mbaya zaidi katika historia ya utawala wa Kizayuni ni mfululizo wa kushindwa kwake katika masuala yanayohusiana na kuporomoka kwa usalama wa ndani kufuatia matukio ya Oktoba 7, vita visivyo na tija na vya kuchosha huko Gaza na kushindwa kimkakati katika makabiliano na Iran. Netanyahu, ambaye awali alijitambulisha kama "mbunifu wa ushindi," sasa amebadilika kuwa "mbunifu wa kushindwa." Mkakati wake dhidi ya Iran, pamoja na jitihada zake za kugawanya nyanja za mapigano, si tu umeambulia patupu, bali pia umeleta matokeo kinyume kabisa na alivyotarajia.

Matokeo yake ni kwamba, utawala wa Kizayuni umejikuta ukikabiliwa na mojawapo ya vita vigumu zaidi katika historia yake, ukiongozwa na waziri mkuu ambaye si tu ameshindwa kupata ushindi, bali pia ameutumbukiza utawala huo katika dimbwi la "kushindwa kwa pamoja" katika kile kinachoitwa kuwa "vita vya maafa makubwa zaidi katika historia yake." Kwa mtazamo wa wakosoaji wake, urithi wa Netanyahu katika historia ya utawala wa Kizayuni si wa ushindi, bali ni mfululizo wa majanga ambayo madhara yake yataendelea kuusumbua utawala huo kwa muda mrefu ujao.