Al-Nujaba ya Iraq yazionya US na Saudia: Shambulio lenu 'mtalilipia gharama kubwa'
Harakat ya Hizbullah al-Nujaba ya Iraq imeonya kwamba maslahi ya Marekani na Saudi Arabia "yatalipa gharama kubwa" baada ya mashambulizi ya pamoja ya anga ya nchi hizo kulenga maeneo ya harakati hiyo ya Muqawama katika mikoa kadhaa ya Iraq usiku wa kuamkia jana, na kuua watu wasiopungua 20 na kujeruhi wengine wengi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, harakati hiyo ya Muqawama ya Iraq ililaani uchokozi wa Marekani na Saudia dhidi ya ardhi ya Iraq baada ya mashambulizi hayo kulenga mikoa mingi, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Baghdad, Basra, Karbala, Kirkuk na Nineveh.
Harakati hiyo imetaka kuondolewa mara moja kambi zote za kijeshi za Marekani na makao makuu ya majeshi ya nchi hiyo katika ardhi ya Iraq, ikielezea uwepo wa jeshi la Marekani kuwa ni "hatari ya kudumu na dhidi ya uwepo" wa usalama na utulivu wa nchi hiyo.
Aidha, iliitaka iliitaka serikali ya Iraq isitishe mara moja ushirikiano wote na Saudi Arabia, ikisisitiza kwamba ufalme huo unatumika kama mfadhili mkuu wa ugaidi dhidi ya Iraq.
Harakati ya Al-Nujaba imekosoa pia mjibizo wa serikali ya Baghdad kwa mashambulizi hayo, ikisema viongozi lazima waachane na "kauli za kudhihirisha hasira na kulaani tu" ambazo zinahamasisha kufanywa uchokozi zaidi.
Al-Nujaba imetoa wito pia wa kupelekwa haraka mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga ili kuilinda anga ya Iraq na imetaka pia kuwepo na uwajibikaji kwa walioshindwa kulinda mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.
Harakati hiyo ya Muqawama imeapa kuwa haitoruhusu Marekani na Saudi Arabia zikiuke mamlaka ya ardhi ya Iraq "bila kulipia gharama kubwa kwa kulengwa maslahi na usalama wao."
Wakati huohuo, Rais wa Iraq Nizar Amedi naye pia amelaani uchokozi huo, akiuelezea kuwa "haukubaliki" na ni "ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Iraq" uliolenga taasisi rasmi za usalama za nchi hiyo kinyume na sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.
Uchokozi wa pamoja uliofanywa na Marekani na Saudi Arabia dhidi ya Iraq umesadifiana na kuwasili mamilioni ya Waislamu kutoka ulimwenguni kote katika mji mtakatifu wa Iraq wa Karbala kuadhimisha Arubaini, ambayo ni kumbukumbu ya kutimia siku ya 40 baada ya kuuawa shahidi Imam Hussain (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, ambao ni moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani.
Baadhi ya wachambuzi wanasema muda uliochaguliwa kufanyia mashambulizi hayo unaashiria uadui dhidi ya mjumuiko huo wa Arubaini, ambao kwa muda mrefu umetumika kama jukwaa la kutangaza mshikamano na Mhimili wa Muqawama na kulaani vita vya Marekani na Israeli na sera zao za kujipanua…/