Malengo ya Julani katika kuanzisha uadui dhidi ya kundi la Hashd al-Shaabi la Iraq
Abu Mohammad al-Julani, mtawala wa serikali ya mpito ya Syria, amedai katika matamshi tatanishi kuwa ana wasiwasi kuhusu uwepo wa makundi ya wanamgambo wa Iraq na vikosi vya Hashd al-Shaabi katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Iraq.
Julani ambaye ni kiongozi wa zamani wa kundi la kigaidi alifanikiwa kuchukua madaraka nchini Syria mwaka 2024 baada ya kuipindua serikali ya Bashar al-Assad, kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo. Sasa, mtawala huyo wa kigaidi nchini Syria anayeungwa mkono na Marekani anadai kuwa na wasiwasi kuhusu uwepo wa Hashd al-Shaabi karibu na mpaka wa nchi hiyo.
Swali linalojitokeza ni, je, ni malengo gani yanafuatiliwa na Julani katika kuelezea wasiwasi huo?
Ukweli ni kwamba, wasiwasi wake hauna msingi wowote wa kitaifa. Kwa maneno mengine ni kuwa hajali lolote kuhusu maslahi ya Syria, la sivyo, angekaribisha uwepo wa vikosi vya Hashd al-Shaabi katika mpaka wa Iraq na Syria, badala ya kutoa matamshi na tuhuma zisizo na msingi dhidi ya kundi hilo la muqawama. Kundi hilo la Iraq linadhamini usalama wa nchi hiyo na lina uzoefu mkubwa katika kukabiliana na vitisho vya kigaidi. Kwa kutoa kauli hiyo ya kichochezi, Julani anajaribu kujipatia uhalali wa kimataifa.
Aidha, Julani ambaye anafanya juhudi za kuondolewa vikwazo dhidi ya Syria, anapanga kwenda sambamba na maslahi ya nchi za Magharibi kwa kuchukua msimamo wa uhasama dhidi ya kundi la muqawama la Iraq. Kwa hakika, kauli hii ni hatua inayolenga kujipendekeza kwa Marekani kwa ajili ya kupata ridhaa ya rais wa nchi hiyo.
Hoja nyingine ni kwamba, kwa kuchukua msimamo dhidi ya Hashd al-Shaabi, Julani anajaribu kuonyesha kuwa muqawama ni tishio la kieneo. Ingawa kauli kama hizo hazibadilishi mtazamo wa kimataifa kuhusu uhalisia wa mtawala huyo kama mtu anayehusishwa na ugaidi, Julani anajaribu kubadilisha nafasi za wanamapambano na magaidi kwa kuituhumu Hashd al-Shaabi kuwa ni tishio la kieneo huku yeye mwenyewe ambaye ndiye gaidi halisi akijidhihirisha kama mtu anayepambana na ugaidi. Msimamo huu unaendana na siasa za Marekani pamoja na mashinikizo ya Washington kwa Baghdad ya kuyataka makundi ya muqawama yaweke chini silaha.
Aidha, Julani ametoa kauli hii wakati maandalizi ya kusaini mkataba wa usalama na utawala wa Kizayuni yakiendelea. Kwa maneno mengine, kwa kuibua tuhuma hizo zisizo na msingi, Julani analenga kuushawishi utawala wa Kizayuni uharakishe makubaliano ya usalama na Syria. Wakati huo huo, kufuatia kuanguka kwa utawala wa Assad, utawala wa Kizayuni umekalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Syria na unakataa kuondoka katika maeneo hayo.
Ikumbukwe pia kwamba kwa kuchukua msimamo dhidi ya kundi muhimu la muqawama wa Iraq, Julani anajaribu kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusiana na vurugu zinazoendelea ndani ya Syria na matukio ya kisiasa nchini humo. Tangu Julani aingie madarakani Syria, takriban watu 15,000 wameuawa kiholela, hakuna dalili zozote za kufanyika uchaguzi hivi karibuni, na ameunda serikali kwa kuwachagua washirika wake wa karibu walio na mitazamo ya kigaidi kama yeye mwenyewe.
Kwa vyo vyote vile, kauli zinazotolewa na watu kama Julani hazitoi changamoto kubwa kwa Harakati ya Mapambano ya Iraq, bali ni mbinu tu ya kupotosha umma kuhusu hali ya ndani ya Syria na tabia ya kigaidi ya Julani mwenyewe, pamoja na jaribio la kujipendekeza kwa Marekani na utawala wa Kizayuni.