Kiongozi mkuu wa kidini wa Bahrain alaani mataifa ya Kiarabu kwa kutumikia ajenda za Marekani na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140384-kiongozi_mkuu_wa_kidini_wa_bahrain_alaani_mataifa_ya_kiarabu_kwa_kutumikia_ajenda_za_marekani_na_israel
Ayatullah Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain, amezilaani nchi za Kiarabu na Kiislamu za kanda ya Magharibi mwa Asia kwa kuchangia katika njama za Marekani na Israel za kuimarisha migawanyiko katika eneo hilo.
(last modified 2026-08-03T10:09:59+00:00 )
Aug 03, 2026 10:08 UTC
  • Ayatullah Sheikh Isa Qassim
    Ayatullah Sheikh Isa Qassim

Ayatullah Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain, amezilaani nchi za Kiarabu na Kiislamu za kanda ya Magharibi mwa Asia kwa kuchangia katika njama za Marekani na Israel za kuimarisha migawanyiko katika eneo hilo.

Akizungumzia yanayojiri hivi sasa katika kanda hiyo na hali ya Umma wa Kiislamu duniani, Sheikh Qassim amekosoa vikali sera za nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu za kufuata kibubusa maagizo ya Washington na Tel Aviv.

"Sio siri kwa serikali yoyote katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni zina misimamo, ajenda na mipango ya kutekeleza njama mbaya. Tunashuhudia utamaduni wenye sumu wa kuzusha migawanyiko kupitia vyombo vyao vya habari kwa lengo la kuvunja umoja wa Umma wa Kiislamu," amesema Ayatullah Sheikh Isa Qassim.

Ameongeza kuwa: "Mbinu kama hiyo inalenga kuzidisha migawanyiko miongoni mwa tawala rasmi katika ngazi za kikanda na kitaifa, kwa kujikita zaidi kwenye nyanja za kidini na kimadhehebu ili kuibua fitina kali zaidi, kuendeleza njama za kuzua matatizo na kuchochea migogoro yenye uharibifu na ya uchochezi."

Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kislamu amesema kwamba rasilimali kubwa za kifedha zinatolewa kwa "mipango hiyo ya njama," ambayo lengo lake ni kuchochea migogoro yenye uharibifu inayoangamiza rasilimali za mataifa ya Kiarabu na Kiislamu na kulenga maisha yao ya pamoja.

Sheikh Isa Qassim amesema kwamba, licha ya kujua njama zinazoendelea kufanyika, idadi kubwa ya nchi za kikanda zinashiriki katika kuchochea migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe huku zikidai kuwa vinatokana na tofauti za kimadhehebu au kidini.

Ameongeza kuwa mwenendo wa nchi hizo ni kuona ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu ukimezwa na migogoro.

"Wanafurahi kuona ulimwengu wa Waarabu na Waislamu ukiteketea, na macho yao hayatatosheka mpaka Waarabu na Waislamu wawe kama watumwa waliofedheheshwa, wakijisalimisha kwa matakwa ya utawala wa dhulma wa Marekani na utawala wa ghasibu wa Israel," amesema Ayatullah Isa Qassim.