Muqawama wa Palestina watoa onyo baada ya mashambulizi mabaya zaidi ya Israel tangu kusitisha mapigano
-
Israel imeua Wapalestina wasiopungua 19 Ukanda wa Gaza.
Makundi ya Muqawama ya Palestina yametoa onyo kali baada ya mashambulizi mabaya zaidi ya anga ya Israel tangu kusitisha mapigano Oktoba 2025, yakisema mashambulizi hayo yasiyokoma ni hujuma ya makusudi dhidi ya makubaliano ya kusitisha mapigano na ujumbe kwamba Israel haina nia ya kutimiza majukumu yake.
Mashambulizi hayo yaliyolenga majengo ya makazi ya raia, magari na mahema yanayohifadhi familia zilizopoteza makazi, yaliua Wapalestina wasiopungua 19 jana Jumapili, na kuhesabiwa kuwa mojawapo ya mauaji ya ya idadi kubwa zaidi ya Wapalestina katika siku moja tangu baada ya kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Madaktari wamesema kwamba miongoni mwa waliouawa wamo wanawake na watoto wadogo.
Watu watatu wa familia moja wameuawa katika shambulio la anga la Israel lilipopiga nyumba ya raia katika Mnara wa al-Sousi magharibi mwa Jiji la Gaza. Waathiriwa wametambuliwa kuwa ni Abdullah Abu Taif, 33, mkewe aliyekuwa mjamzito, Abeer Anan, 29, na mtoto wao wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka mitano, Azzam.
Vyanzo vya matibabu vimeripoti kuwa, katika eneo la al-Qarara, kaskazini magharibi mwa mji wa Khan Yunis huko kusini mwa Ukanda wa Gaza, shambulio la Israel dhidi ya nyumba moja limemuua shahidi Mahmoud al-Hams aliyekuwa na umri wa miaka 38, mkewe Fatima, (37), na binti yao mdogo.
Mashambulizi haya yamelaaniwa vikali na makundi ya mapambano ya Palestina, ambayo yameushutumu utawala wa Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kutaka kudhoofisha juhudi za kutekeleza makubaliano hayo.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imeulaani utawala huo kwa kuzidisha mashambulizi ya kikatili katika njama za kutaka kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Hamas imetoa wito kwa wapatanishi na wadhamini wa makubaliano hayo kuishinikiza Tel Aviv ili isimamishe mashambulizi yake na kuheshimu makubaliano hayo.
Vilevile, Kamati za Harakati za Muqawama za Palestina, muungano wa makundi ya mapambano, imelaani mashambulizi hayo, na kuyataja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano na jaribio la kulazimisha "ukweli mpya ardhini."