Kwa nini shambulio la Saudi Arabia na Marekani dhidi ya Hashd al-Shaabi ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Iraq?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140392-kwa_nini_shambulio_la_saudi_arabia_na_marekani_dhidi_ya_hashd_al_shaabi_ni_ukiukaji_wa_wazi_wa_mamlaka_ya_kujitawala_ya_iraq
Kikosi cha Hashd al-Shaabi cha Iraq kilitangaza siku chache zilizopita kuwa watu wasiopungua 20 waliuawa na wengine 32 kujeruhiwa katika shambulio la pamoja la kichokozi lililofanywa na Marekani na Saudi Arabia dhidi ya Iraq mapema Jumatano iliyopita.
(last modified 2026-08-03T11:17:39+00:00 )
Aug 03, 2026 11:09 UTC
  • Kwa nini shambulio la Saudi Arabia na Marekani dhidi ya Hashd al-Shaabi ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Iraq?

Kikosi cha Hashd al-Shaabi cha Iraq kilitangaza siku chache zilizopita kuwa watu wasiopungua 20 waliuawa na wengine 32 kujeruhiwa katika shambulio la pamoja la kichokozi lililofanywa na Marekani na Saudi Arabia dhidi ya Iraq mapema Jumatano iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo la muqawama la Iraq ilisema: "Wakati wa kufanyika vitendo hivi vya kichokozi, kambi za Hashd al-Shaabi katika mikoa ya Baghdad, Wasit, Nineveh, Basra, Kirkuk, Karbala na Diyala zilishambuliwa, ambapo mbali na kusababisha maafa vilisababisha pia uharibifu wa mali katika makao makuu, magari na vifaa vya kijeshi."

Huku ikiliita shambulio hilo kuwa la kigaidi, taarifa hiyo iliendelea kusisitiza kuwa shambulio hilo linaongeza " hatari," ni "ukiukwaji wa mamlaka na kujitawala kwa Iraq," na ni "hatua dhidi ya taasisi rasmi za usalama wa nchi."

Kwa madai ya Riyadh na Washington, operesheni hiyo ilifanywa katika kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya ndege zisizo na rubani kwenye vituo vya mafuta vya Saudia.

Awali, siku ya Jumatatu na Jumanne, Saudi Arabia iliripoti kuzuia na kutungua ndege zisizo na rubani, ikidai kuwa zilikuwa zimeelekezwa kutokea Iraq zikilenga miundombinu ya mafuta ya ufalme huo.

Kufuatia mashambulizi ya Marekani na Saudi Arabia dhidi ya kambi kadhaa za Hashd al-Shaabi, Waziri Mkuu wa Iraq aliitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyo, ambapo mbunge wa Iraq, Faleh al-Khazali, alisisitiza kuwa, "mashambulizi dhidi ya ngome za vikosi vyetu vya usalama ni uchokozi wa wazi na ukiukwaji wa mamlaka ya kujitawala Iraq. Serikali ya Iraq na Waziri Mkuu wake wana wajibu wa kutetea kwa ujasiri usalama wa watu wa Iraq na maslahi ya taifa lao."

Uchokozi wa kijeshi wa pamoja wa Saudi Arabia na Marekani dhidi ya Iraq, bila kujali visingizio vilivyotolewa, ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya nchi hiyo. Isitoshe, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa, mashambulizi hayo ya kichokozi hayawezi kuhalalaishwa kwa vyovyote vile kwa sababu zifuatazo:

1. Uchokozi dhidi ya jeshi rasmi la nchi bila uratibu na serikali ya Iraq

Vikosi vya Hashdul al-Shaabi si kundi la wanamgambo tena. Chini ya sheria za Iraq, vimeingizwa katika muundo rasmi wa jeshi la nchi hiyo na vinafanya kazi chini ya amri ya Amiri Jeshi Mkuu. Hivyo, shambulio lolote dhidi yake linachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya taasisi ya kijeshi ya taifa huru. Serikali ya Iraq imesema waziwazi kuwa haikuarifiwa wala kutoa idhini ya kufanyika shambulio hilo.

Kufanyika operesheni za kijeshi ndani ya eneo la nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa bila taarifa na idhini ya serikali ya nchi hiyo bila shaka ni kitendo cha uchokozi na uingiliaji wa mambo yake ya ndani.

2. Uhalalishaji wa kisheria usio na msingi na matumizi mabaya ya "haki ya kujilinda."

Marekani na Saudi Arabia zimedai kuwa mashambulizi hayo yalifanyika katika kujibu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yaliyofanywa kutokea katika ardhi ya Iraq na kwamba yalizingatia Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa (haki ya kujilinda). Madai haya hayaendani kabisa na viwango vya sheria za kimataifa kwa sababu kadhaa:

- Masharti ya uwiano na haja ya dharura hayakuzingatiwa. Hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha kuwepo kwa tishio la karibu ambalo lingehalalisha hatua ya haraka na kubwa kama hiyo.

 - Sharti la kutoa taarifa kwa Baraza la Usalama ambalo ni sharti la msingi kabla ya kutumia haki ya kujilinda, halikutimizwa, bali hatua ya upande mmoja ilichukuliwa bila idhini ya baraza hilo.

- Haki ya kujilinda inahusu nchi iliyofanya shambulio, na sio makundi yaliyoko katika ardhi ya nchi ya tatu. Kama madai hayo yangethibitika, sheria inasema kwamba serikali ya Iraq ingetaarifiwa ili ichukue hatua zinazostahili, badala ya kuchukuliwa hatua za kijeshi za upande mmoja kuhusu suala hilo.

3. Ukiukwaji wa mamlaka ya kujitawala na utulivu wa Iraq na kuchochea zaidi mgogoro wa kikanda

Kitendo hiki cha uchokozi, na ulazima wa kukijibu, vinafungua mlango wa kuchukuliwa hatua zaidi za kijeshi katika eneo. Mbali na hayo, hatua kama hizo zinadhoofisha imani kwa serikali ya Iraq katika kudumisha usalama wa ndani na kuharibu mchakato wa kisiasa pamoja na juhudi za maridhiano ya kitaifa nchini humo.

Kwa hakika, shambulio la pamoja la Marekani na Saudi Arabia dhidi ya Vikosi vya Hashd al-Shaabi si tu kwamba haliwezi kuhalalishwa kisheria, bali pia lina madhara makubwa kwa usalama wa eneo zima. Hatua hii ni mfano dhahiri wa kuchukuliwa maamuzi ya upande mmoja na kupuuzwa sheria za msingi za kimataifa, ambapo jamii ya kimataifa inapaswa kukemea uchokozi huu na kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala ya Iraq na kutatuliwa migogoro kwa njia za amani.