Vikosi vya Yemen vyashambulia shabaha muhimu ndani ya Uwanja wa Ndege wa Najran, Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140424-vikosi_vya_yemen_vyashambulia_shabaha_muhimu_ndani_ya_uwanja_wa_ndege_wa_najran_saudi_arabia
Jeshi la Yemen limekishambulia kituo cha kimkakati ndani ya uwanja wa ndege wa Najran kusini mwa Saudi Arabia, ikiwa ni jibu kwa mashambulizi na mzingiro unaoendelea kufanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2026-08-05T02:57:28+00:00 )
Aug 05, 2026 02:55 UTC
  • Vikosi vya Yemen vyashambulia shabaha muhimu ndani ya Uwanja wa Ndege wa Najran, Saudi Arabia

Jeshi la Yemen limekishambulia kituo cha kimkakati ndani ya uwanja wa ndege wa Najran kusini mwa Saudi Arabia, ikiwa ni jibu kwa mashambulizi na mzingiro unaoendelea kufanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema kuwa jeshi la nchi hiyo jana Jumanne lililenga shabaha hiyo muhimu nchini Saudia kwa kutumia ndege isiyo na rubani ya kujilipua iliyotengenezwa nchini humo.

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema shambulio la kulipiza kisasi limetimiza malengo yaliyokusudiwa.

Amesisitiza kuwa Jeshi la Yemen limekishambulia kituo cha kimkakati ndani ya uwanja wa ndege za Najran kusini mwa Saudi Arabia ili kulipiza kisasi hatua ya Riyadh ya kukiuka anga ya Yemen katika majimbo ya kaskazini ya Sa’ada na Hajjah kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

"Tunamuonya adui Saudia kwamba hatua yake yoyote ya kukiuka anga yetu haitaachwa bila jibu au adhabu," amesisitiza msemaji wa Jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree.

Tarehe 20 Julai, serikali ya Sana’a ilitangaza mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia, ikisema kuwa mamlaka za Riyadh zimetekeleza “mzingiro usio wa haki na wa kukandamiza” dhidi ya watu wa Yemen kwa karibu miaka 12, huku “zikipora rasilimali na kuiwekea nchi hiyo mzingiro kamili.”

Tangu wakati huo, Jeshi la Yemen lilisema kuwa limeanzisha mashambulizi dhidi ya meli za Saudi Arabia katika Bahari Nyekundu.

Saudi Arabia na washirika wake wa Kiarabu walianzisha mzingiro dhidi ya Yemen kama sehemu ya vita kamili tangu mwezi Machi 2015, kwa uungaji mkono wa kijeshi, kisiasa na kiutendaji wa Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.