Ghaza yafanya maziko makubwa zaidi ya halaiki ya Wapalestina 112 waliouliwa kikatili na Israel
Wapalestina wamewazika watu 112 wa ukoo mmoja waliouawa katika mashambulizi ya kinyama ya anga yaliyofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel mnamo Novemba 2023, baada ya mabaki yao kupatikana kutoka chini ya vifusi mwezi uliopita.
Jamaa wa familia ya Abu Shari'a na al-Hasayna walikusanyika katika Jiji la Ghaza jana Jumanne kuwaaga kwa mara ya mwisho wapendwa wao, ambao miili yao ilikuwa imepangwa safu zilizofunikwa bendera za Palestina.
Kwa wengi, ulikuwa wakati wa hali zote mbili za faraji na huzuni mpya baada ya karibu siku 1,000 za kusubiri kupata miili ya jamaa zao.
"Kuna hisia ya maumivu na furaha," alisema Amer Abu Shari'a, ambaye alipoteza jamaa katika shambulio hilo.
"Furaha kwa sababu tutawazika na kuwaenzi Mashahidi hawa baada ya miaka mitatu. Lakini huzuni imerejea, kana kwamba mauaji hayo yametokea leo."
Shambulio hilo la kinyama lililofanywa na jeshi la kizayuni katika kitongoji cha Sabra lilikuwa moja ya matukio mabaya zaidi ya kuuawa kwa wingi mkubwa wananchi madhulumu wa Palestina katika shambulizi moja tu la mauaji ya kimbari yaliyoendelea kwa muda wa miaka miwili.
Ndege za kivita za Israel zilibomoa na kusawazisha na ardhi jengo zima la makazi ambapo mamia ya watu wa ukoo wa Abu Shari'a na al-Hasayna walikuwa wakiishi na kupata hifadhi ndani yake.
Zaidi ya watu 300 waliuawa, wakiwemo watoto 44, wanawake 37 na zaidi ya watu 10 wenye ulemavu.
Akthari yao walibaki wamezikwa chini ya majengo yaliyoporomoka.
Juhudi za kuipata miili kutoka kwenye vifusi zilisitishwa katika miezi ya mwanzo ya vita kwa sababu timu za utafutaji na uokoaji hazikuwa na vifaa vizito vinavyohitajika kwa ajili ya operesheni hiyo, ambavyo vilikuwa vimeharibiwa au kuzuiliwa na jeshi la kizayuni visiingizwe Ghaza.
Wafanyakazi wa Ulinzi wa Raia walianzisha tena operesheni ya kulitafuta eneo hilo mnamo Julai 14 kwa kutumia vifaa vichache na visivyo na uwezo wa kutosha.
Maafisa walisema nguvu ya miripuko hiyo ilikuwa imetawanya mabaki ya miili ya binadamu, na kuifanya operesheni ya uokoaji kuwa ngumu zaidi.
Hadi kufikia tarehe Mosi Agosti, wafanyakazi wa Ulinzi wa Raia walikuwa wamepata mabaki ya watu 112, huku waathiriwa zaidi wakiaminika kuzikwa chini ya vifusi.
"Tulifanya kazi kwa siku 17 ili kuipata miili hiyo katika hali ngumu sana. Mwishowe, tulifanikiwa kupata mabaki ya watu 112," ameeleza Mahmoud Basal, msemaji wa Ulinzi wa Raia wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza.
"Maelfu ya watu bado wamezikwa chini ya vifusi, huku familia zao zikiendelea kuomboleza na kuomba njia za kuziokoa", ameongezea kueleza Basal…/