Jeshi la Yemen lapiga meli nyingine ya mafuta ya Saudi Arabia katika Bahari Nyekundu
-
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree
Jeshi la Yemen limeishambulia meli ya mafuta ya Saudi Arabia katika sehemu ya kaskazini ya Bahari Nyekundu, baada ya meli hiyo kukiuka mzingiro wa baharini uliowekwa dhidi ya Saudi Arabia.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, ameeleza kuwa meli hiyo ya mafuta kwa jina la Wafa, imeshambuliwa kwa makombora kadhaa ya balistiki karibu na pwani ya Yanbu na kwamba shambulio hilo lililenga shabaha kwa usahihi."
Brigedia Jenerali Saree ameongeza kuwa: Jeshi la Yemen limefanya operesheni hiyo "ili kuweka mzingiro wa baharini dhidi ya adui Saudia" na kuimarisha kile alichosema ni mlinganyo wa "mzingiro kwa mzingiro."
Amefafanua kuwa, shambulio hilo limefanya jumla ya meli za mafuta za Saudi Arabia zilizolengwa tangu kutangazwa mzingiro huo tarehe 22 mwezi Julai kufikiria nane.
Msemaji wa Jeshi la Yemen pia amesema: Meli 29 za mafuta za Saudi Arabia zimezuiwa kuendelea na safari na kulazimishwa kurudi nyuma katika Bahari Nyekundu na katika bahari ya Uarabuni.
"Saudi Arabia ilikuwa imeanza kuelekeza meli zake za mafuta upande wa kaskazini mwa Bahari Nyekundu kufuatia kuimarishwa mzingiro wa majini katika Lango-Bahari la Bab al-Mandab na jeshi la Yemen linathibitisha kuwa operesheni zake zitaendelea na zitashadidisha mashambulizi dhidi ya meli za mafuta za Saudi Arabia kaskazini mwa Bahari ya Shamu ili kufunga njia zote za kufikia eneo hilo na kuzuia meli hizo kupita," ameeleza Msemaji wa jeshi la Yemen.