Malengo yanayofuatiliwa na Marekani katika kuzichochea nchi za Kiarabu zikabiliane na Iran
Hata kama nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi hazitaki kuchochea mivutano katika eneo, kwa mujibu wa sera zao rasmi, lakini Marekani inajaribu kuzivuta katika makabiliano ya moja kwa moja na Iran.
Jambo muhimu ambalo limejitokeza katika wiki za karibuni ni kwamba, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, kwa sasa Israel haishiriki waziwazi katika vita dhidi ya Iran, ambapo ripoti kadhaa zinadai kuwa Marekani imekataa ombi la utawala huo wa kibaguzi la kushiriki moja kwa moja katika mgogoro huu. Haya yanaripotiwa licha ya kuwepo dalili chungu nzima zinazoonyesha kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni zote mbili zimeazimia kuchochea nchi za Kiarabu ili zishiriki kwenye vita dhidi ya Iran.
Ingawa kumekuwepo na ripoti na habari kuhusu kuhusika kwa siri kwa baadhi ya nchi za Kiarabu katika vita vya siku 40 dhidi ya Iran, nchi hizo hazijawahi kukiri rasmi kushiriki kwao katika mgogoro huu na kwa ujumla zimejaribu kuepuka madhara yake. Swali linalojitokeza ni je, ni malengo gani yanafuatiliwa na Marekani katika kuzisukuma nchi za Kiarabu katika makabiliano na Iran?
Moja ya malengo makuu ya Marekani ni kupata faida halisi kutokana na vita dhidi ya Iran. Malengo ya kimkakati yaliyochochea kuanzishwa mgogoro huu ni kutaka kuuangusha mfumo wa kisiasa wa Iran na kusambaratisha umoja wa ardhi yake. Pamoja na hayo, si tu kwamba malengo haya hayajafikiwa, bali Iran, licha ya mashinikizo makali ya Marekani, inaendelea udhibiti kikamilifu Lango-Bahari la Hormuz. Kwa hakika, lengo la Marekani kuhusiana na mzozo huu limepungua na kubakia kuwa ni kutaka kufunguliwa tu Lango-Bahari la Hormuz. Kushindwa huku kumezua ukosoaji mkubwa dhidi ya utawala wa Trump, ndani ya nchi na kimataifa. Katika mazingira haya, Marekani inajaribu kuziburuza nchi za Kiarabu kwenye mzozo na Iran, hatua inayolenga angalau kupanda mbegu za migawanyiko, kuchochea mivutano na kuharibu uhusiano wa Iran na nchi za eneo, licha ya ukweli kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuwepo uhusiano mzuri na majirani zake na imekuwa ikitekeleza kikamilifu sera ya kupanua uhusiano huo katika miaka ya karibuni.
Lengo jingine muhimu la Marekani ni kubadili sura ya mzozo na Iran kutoka kuwa makabiliano kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni na kuwa vita vikubwa vya eneo, vita ambavyo vitahusisha nchi za Kiislamu. Kwa mtazamo wa Marekani, mabadiliko haya ya kijeshi kuhusiana na mzozo huu yanaweza kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran huku yakiandaa fursa kwa Marekani kuuza silaha zaidi kwa nchi za Kiarabu. Kwa maneno mengine, ajenda ya Marekani ni kunyonya utajiri na rasilimali za nchi za Kiarabu kwa kujaribu kuidhihirisha Iran kama tishio. Ingawa Marekani ilishawahi kutumia sera hii huko nyuma, lakini uwezo wa sasa wa kijeshi wa Iran ukilinganishwa na ule wa Marekani umeifanya Washington isisitize zaidi kuhusu tishio la Iran kwa mataifa ya Kiarabu, kuliko wakati mwingine wowote. Hii ni licha ya ukweli kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mara kwa mara kuwa uwezo wake wa kijeshi ni wa kujilinda na imethibitisha kivitendo kuwa haitaanzisha vita dhidi ya taifa lolote la Kiislamu. Lengo la tatu la Marekani ni kuhudumia maslahi ya Israel katika eneo. Kufuatia kurejea kwa Trump madarakani, utawala wa Kizayuni umekuwa ukifuatilia upanuzi wa Makubaliano ya Abraham na kuanzishwa uhusiano wa kawaida na nchi zaidi za Kiarabu, lengo ambalo bado halijafikiwa hadi sasa. Hivyo, kudhoofisha uhusiano wa Iran na nchi za Kiarabu kunahudumia maslahi ya utawala wa Kizayuni, na ndio maana unachangamkia sana njama ya kuzivuta nchi za Kiarabu katika vita dhidi ya Iran.