Mkuu wa Mossad awatimua maafisa wawili wakuu kwa kufeli mpango wa kuipindua serikali ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140486-mkuu_wa_mossad_awatimua_maafisa_wawili_wakuu_kwa_kufeli_mpango_wa_kuipindua_serikali_ya_iran
Mkuu wa shirika la ujasusi na ugaidi la utawala wa kizayuni wa Israel Mossad, Roman Gofman, amewafukuza kazi maafisa wawili wakuu wa intelijensia baada ya kushindwa au kutotekelezwa mpango wa kuipindua serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-09-05T16:25:28+00:00 )
Aug 07, 2026 12:29 UTC
  • Mkuu wa Mossad awatimua maafisa wawili wakuu kwa kufeli mpango wa kuipindua serikali ya Iran

Mkuu wa shirika la ujasusi na ugaidi la utawala wa kizayuni wa Israel Mossad, Roman Gofman, amewafukuza kazi maafisa wawili wakuu wa intelijensia baada ya kushindwa au kutotekelezwa mpango wa kuipindua serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha Israel cha Chaneli ya 12, maafisa hao waliotimuliwa ni mkuu wa kurugenzi ya intelijensia, ambaye aliteuliwa miezi michache tu iliyopita, na mkuu wa kitengo cha Iran cha shirika hilo la ujasusi la Israel.

Kituo hicho cha televisheni cha12 kimebainisha kuwa, mpango huo wa kuipindua serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulipangwa kwa uratibu na Marekani ukilenga kuchochea harakati za ndani ya nchi dhidi ya serikali, ikiwa ni pamoja na kuyaunga mkono makundi ya upinzani, kupitia mashambulizi makubwa ya anga ya kijeshi yaliyoanzishwa kwa pamoja na utawala wa kizayuni na Marekani.

Chaneli ya 12 ya televisheni ya Israel, imenukuu tathmini zilizofanywa kuhusu suala hilo na kueleza kwamba, mpango huo itakuwa ama ulifeli au haukufikia hatua ya utekelezaji.

Vyanzo vya masuala ya usalama vimeiambia chaneli hiyo ya utawala wa kizayuni kwamba uhusiano wa Gofman na maafisa hao wawili ulikuwa umedorora tangu mwanzo, na kuongeza kuwa kufukuzwa kazi watu hao kulijiri wakati wa mabadiliko makubwa ya uongozi yaliyofanywa na Mossad na kuhusu vipaumbele vyake, hususan kuhusiana na Iran.

Kituo hicho cha utangazaji kimenukuu pia ripoti za kimataifa zikisema, mpango huo ulikuwa umejumuisha sinario za kubadilisha uongozi wa Iran na kufanya uratibu na maafisa wa Marekani katika awamu ya "baada ya utawala" uliopo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mpango wa pamoja wa Mossad na shirika la ujasusi la Marekani, CIA ulihusisha wanamgambo wa Kikurdi wanaoingia Iran huku wakipatiwa usaidizi wa anga wa Marekani na Israel ili kuiondoa serikali ya Iran na kuweka viongozi wengine madarakani.

Hata hivyo, kwa mujibu wa chaneli ya 12 ya televisheni ya utawala haramu wa Israel, juhudi hizo zilisimama katika hatua za awali, na kupelekea kutolewa pendekezo la kuahirishwa, na wale waliohusika kuwajibishwa.

Itakumbukwa kuwa Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu alikiri mnamo Machi 13 kwamba ingekuwa vigumu kuipindua serikali ya Iran, akisema "hakuna uhakika kama hili litatokea"…/