UNICEF yachukua hatua dhidi ya afisa anayetuhumiwa kufanya ujasusi kwa maslahi ya Israel
-
Yahav Lechner, mkurugenzi wa ofisi ya UNICEF Washington, D.C
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amethibitisha kwamba Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linachukua hatua dhidi ya mmoja wa wafanyakazi wake, kufuatia madai kwamba alifanya ujasusi kwa maslahi ya Israel wakati wa kazi yake ya awali katika Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa.
Afisa husika wa UN, Yahav Lechner, ni mkurugenzi wa ofisi ya UNICEF huko Washington, D.C., na inasemekana amewekwa katika likizo ya kiutawala.
Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema akijibu swali kuhusu madai hayo kwamba, "UNICEF ina habari kuhusu madai hayo mazito dhidi ya mmoja wa wafanyakazi wake na inachukua hatua zinazofaa."
Ameongeza kuwa vitendo hivi, ikiwa madai hayo ni ya kweli, ni ukiukaji wa majukumu ya wafanyakazi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kanuni za wafanyakazi na viwango vya kimataifa vya maadili ya utumishi wa umma, ambavyo vinasisitiza kwamba majukumu ya wafanyakazi wa shirika hilo ni ya kimataifa, si ya kitaifa, na yanawataka wawe huru na wasioegemea upande wowote.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa na tovuti huru ya Marekani ya DropSite News, Lechner inadaiwa aliwapa wanadiplomasia wa Israel taarifa za siri, rasimu ambazo hazijachapishwa na maelezo ya mikutano ya faragha wakati wa kazi yake katika Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa kati ya 2014 na 2015.
Uchunguzi huo ulitokana na barua pepe zilizovujishwa na kundi la udukuzi la "Hanzala" na kuchapishwa na jukwaa la "Distributed Denial of Secrets".
Barua pepe hizo zinajumuisha mawasiliano yaliyohusishwa na Ron Prosor, balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa kati ya 2011 na 2015. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, moja ya barua hizo inaonyesha jinsi taarifa za ndani zilivyochochea hatua za Israel katika Bunge la Marekani.
Mawasiliano haya yanarejea katika kipindi ambacho Israel ilikabiliwa na mashinikizo ya kimataifa kufuatia uvamizi wake wa 2014 dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambao ulisababisha mauaji ya karibu Wapalestina 2,322 na kujeruhi wengine 11,000, pamoja na uhalifu wake mkubwa katika Ukingo wa Magharibi.