Malaysia na Indonesia zasisitiza kuunga mkono Palestina na maeneo matakatifu Baytul-Muqaddas
-
Malaysia na Indonesia zasisitiza kuunga mkono Palestina na maeneo matakatifu Baytul-Muqaddas
Malaysia na Indonesia kwa mara nyingine tena zimesisitiza uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina na kuhifadhi hadhi ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika Baytul-Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Sisitizo hilo limetolewa katika mkutano wa mawaziri kuhusu kuunga mkono Baytul-Muqaddas na maeneo matakatifu uuliofanyika huko Amman, mji mkuu wa Jordan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia imetangaza: "Quds ni sehemu muhimu ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na inakataa jaribio lolote la kubadilisha hadhi ya kisheria, kihistoria, idadi ya watu na kidini ya mji huu.
Malaysia pia imelaani mashambulizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na upanuzi wa vitongoji haramu unaofanywa na utawala wa Kizayuni. Kuala Lumpur pia imesisitiza uungaji mkono wake kwa ajili ya kuanzishwa taifa huru la Palestina.
Kwa upande mwingine, Indonesia imetoa wito wa umoja kutoka kwa jamii ya kimataifa dhidi ya vitendo vya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Armanatha Nasir, amekosoa kimya cha jamii ya kimataifa dhidi ya ukiukwaji wa haki za Palestina na akasema: Jamii ya kimataifa haipaswi kuhitalifiana na kugawanywa katika kukabiliana na vitendo hivi.
Indonesia pia imesisitiza hitajio la utambuzi mpana wa hali ya Palestina, kuimarisha ulinzi wa Msikiti wa Al-Aqswa, kusaidia ujenzi mpya wa Gaza, kupiga jeki mchakato wa maridhiano ya kitaifa ya Palestina, na kuunga mkono shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutoa Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).