Mustakabali wa usalama wa eneo: Kwa nini nafasi muhimu ya nchi za kanda ni ya dharura?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140580-mustakabali_wa_usalama_wa_eneo_kwa_nini_nafasi_muhimu_ya_nchi_za_kanda_ni_ya_dharura
Pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya kutetea Quds Tukufu (Jerusalem), uliofanyika mjini Amman, Jordan, Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, alisisitiza umuhimu wa kuandaliwa dira ya pamoja ya Kiarabu kwa ajili ya mustakabali wa usalama wa eneo. Alisema kuwa nchi za eneo lazima ziwe katika mstari wa mbele wa kubuni mipango yoyote ya usalama katika siku zijazo.
(last modified 2026-08-11T07:42:38+00:00 )
Aug 11, 2026 07:25 UTC
  • Mustakabali wa usalama wa eneo: Kwa nini nafasi muhimu ya nchi za kanda ni ya dharura?

Pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya kutetea Quds Tukufu (Jerusalem), uliofanyika mjini Amman, Jordan, Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, alisisitiza umuhimu wa kuandaliwa dira ya pamoja ya Kiarabu kwa ajili ya mustakabali wa usalama wa eneo. Alisema kuwa nchi za eneo lazima ziwe katika mstari wa mbele wa kubuni mipango yoyote ya usalama katika siku zijazo.

Abdelatty alisisitiza kuwa Misri inaamini kwamba usalama wa eneo unapaswa kudhaminiwa na nchi za eneo hili hili, na kwamba mipango ya siku zijazo lazima izingatie maslahi ya serikali za kanda hii. Msimamo huu uliotangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri umewahi pia kusisitizwa na viongozi wa nchi tofauti za eneo. Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia wamesisitiza mara kwa mara kuwa usalama wa Asia Magharibi unapaswa kudhaminiwa na mataifa ya eneo hili yenyewe. Ingawa hadi sasa nchi za Kiarabu kwa kiasi kikubwa zimepuuza suala la usalama wa ndani ya eneo unaosimamiwa na mataifa husika, swali linajitokeza kuwa je, kwa nini baadhi ya nchi za Kiarabu, ikiwemo Misri yenyewe, sasa zimeamua kuwa ni muhimu kuandaliwa mipango ya usalama wa siku zijazo inayozingatia mahitaji ya mataifa ya eneo?

Matukio ya miaka mitatu iliyopita, hasa jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Palestina, Syria, Lebanon, Yemen, Iran, na hata Iraq, yanaweza kutajwa kama sababu kuu ya sisitizo hili la kudhaminiwa usalama wa eneo na nchi za eneo hili zenyewe. Kwa hakika, jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni na Marekani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita zimepelekea kueleweka zaidi asili ya vitisho vilivyopo. Kinyume na propaganda za uongo zinazoenezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni kwamba Iran ni tishio kwa eneo, utawala wa Kizayuni wenyewe ndio tishio kuu katika eneo hili. Katika miaka mitatu iliyopita, sambamba na kufanya ukatili wa kutisha dhidi ya mataifa ya eneo, utawala huo umevamia na kukalia kwa mabavu maeneo zaidi ya Waarabu, huku waziri mkuu wake na mawaziri wa baraza lake la mawaziri wakitetea waziwazi uanzishwaji wa "Israel Kubwa." Katika mazingira haya, kutegemea nguvu za nje, hasa Marekani, kwa ajili ya usalama hakutadhamini kwa vyovyote vile usalama wa mataifa ya Kiarabu, bali kutashusha usalama wao hadi kiwango cha chini kabisa.

Imedhihirika katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwamba, kwa upande wa Marekani, mataifa ya Kiarabu yana hadhi ya chini zaidi yakilinganishwa na Israel.

Sababu ya pili inahusu uendelevu na uhalali wa mipango ya usalama ndani ya eneo husika. Uzoefu umeonyesha kuwa mipango ya usalama iliyoandaliwa bila ushiriki wa dhati wa nchi za eneo huwa haina uthabiti wowote. Kinyume chake, nchi za eneo zenyewe zinapochukua jukumu la kubuni na kudhamini usalama wao, mipango hiyo hupata uhalali mkubwa zaidi, na hivyo kuimarisha utayari wa mataifa hayo katika kuheshimu na kuitekeleza. Mifumo ya usalama ambayo imekuwa ikisimamia usalama wa nchi nyingi za Asia Magharibi imeegemezwa zaidi kwa Marekani. Hata hivyo, matokeo yake yamekuwa ni kuupa utawala wa Kizayuni uhuru kamili wa kufanya uchokozi na ukatili dhidi ya mataifa asili ya eneo, huku pia ikifungua mlango wa Marekani na utawala wa Kizayuni kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mashambulizi kama hayo yanaweza pia kuelekezwa kirahisi dhidi ya nchi za Kiarabu iwapo kutatokea mzozo kati yazo na utawala wa Kizayuni, ikizingatiwa kuwa utawala huo unaoungwa mkono kikamilifu na Marekani, unajaribu kuvuruga uwiano wa nguvu na kujiimarisha kama nguvu kuu katika eneo.

Sababu ya tatu inayofafanua umuhimu wa kubuniwa mifumo ya usalama ya siku zijazo inayozingatia maslahi ya mataifa ya eneo ni kupunguza gharama za usalama. Nchi za eneo hili hutumia kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kwa ajili ya kununua silaha kutoka kwa nchi za Magharibi katika jitihada za kujidhaminia usalama. Kuanzisha mfumo wa pamoja wa usalama unaozingatia maslahi ya mataifa ya eneo kunaweza kuzuia mashindano ya gharama kubwa ya kujilimbikizia silaha, huku kukielekeza rasilimali za kifedha kwenye maendeleo ya kiuchumi na ustawi.

Hatimaye, kubuni mipango ya usalama ya ndani ya eneo kunaweza kusaidia pia kupunguza vitisho, jambo muhimu sana kwa Asia Magharibi, eneo ambalo halijapata amani wala utulivu tangu mwaka 2011 kutokana na uingiliaji wa mataifa ya kigeni na mifumo ya usalama inayotoka nje ya eneo hili.