UN: Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel umeshafikia “hatua ya kusambaratika”
Mratibu wa juhudi za Umoja wa Mataifa za mchakato wa amani Mashariki ya Kati, Ramiz Alakbarov, amesema Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel umefikia “hatua ya kusambaratika”, huku ongezeko la vitendo vya ukatili na mabavu vya walowezi wa Israel, upanuzi wa vitongoji haramu na ufurushwaji wa jamii za Wapalestina vikiibadilisha kwa kasi sura ya eneo hilo.
Alakbarov ameyasema hayo alipohutubia kikao cha wazi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kubainisha kuwa, hali hiyo si matokeo ya uzorotaji wa ghafla, bali ni zao la miongo kadhaa ya mzozo ambao umeendeleza ukaliaji wa Israel na kudhoofisha matarajio ya kuanzishwa taifa huru la Palestina.
“Ukingo wa Magharibi umefikia hatua ya kusambaratika,” Alakbarov ameonya, akisema hatua zinazoendelea kuchukuliwa zinayafanya matarajio ya kuwa na dola huru la Palestina lenye mamlaka na linaloweza kujiendesha, kuwa magumu zaidi kila siku.
Tangu Januari 2023, jamii 127 za Wapalestina zimefurushwa, kwa sehemu au kikamilifu, huku karibu familia 50 zikihamishwa kikamilifu na kuathiri zaidi ya watu 6,390. Mwaka 2026 pekee, takribani Wapalestina 3,800, karibu nusu yao wakiwa watoto, wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na ukatili wa walowezi, ubomoaji wa nyumba zao na kufukuzwa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), kuanzia pale vilipoanza vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023 hadi 24 Julai 2026, Wapalestina 1,122 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, wakiwemo 76 mwaka huu.
Katika kipindi hicho, mashambulizi ya walowezi yameongezeka kwa kiwango ambacho Umoja wa Mataifa umekielezea kuwa hakijawahi kushuhudiwa.
“Haya si matukio yaliyotengwa,” Alakbarov amesema. “Ni hatua zinazohusiana, ambazo zinaubadilisha Ukingo wa Magharibi, zinadhoofisha utawala wa Palestina na kuendeleza unyakuzi wa eneo hilo kwa vitendo”.
Umoja wa Mataifa umeonya pia kuhusu kasi ya upanuzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa kizayuni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.../