Israel inashikilia waandishihabari 40 wa Kipalestina katika kampeni ya kubana sauti ya haki
-
Wafungwa wa Kipalestina katika Gereza la Ketziot, katika maeneo ya kusini yanayokaliwa kwa mabavu, Februari 26, 2025. (Picha na Flash90)
Israel inawashikilia takriban waandishi wa habari 40 wa Kipalestina, wakiwemo wanawake watano, huku ikiongeza kasi ya ukandamizaji mkubwa ili kunyamazisha vyombo vya habari vya Kipalestina na kuzuia kuripotiwa kwa ukiukaji na jinai zake. Hayo ni kwa mujibu wa Jumuiya ya Wafungwa wa Kipalestina (PPS).
Jumuiya hiyo imesema utawala wa Israel pia umewaweka waandishi wa habari watatu chini ya kizuizi cha nyumbani, wakati 19 kati ya wale wanaoshikiliwa sasa wanazuiliwa chini ya “kizuizi cha utawala” bila kufunguliwa mashtaka au kufikishwa mahakamani.
Zaidi ya waandishi wa habari 250 wa Kipalestina wamekamatwa au kuzuiliwa tangu Israel ilipoanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023, kundi hilo limesema, huku wengi wao wakiachiliwa baadaye.
Kulingana na takwimu za PPS, zaidi ya waandishi wa habari 260 pia wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo.
Kundi hilo limesema kuwa ukamataji, mauaji, na kupotea kwa nguvu kwa waandishi wa habari wa Kipalestina ni sehemu ya kampeni ya kimfumo ya Israel ya kuinyamazisha tasnia ya habari, kusambaratisha uhuru wa vyombo vya habari, na kuuzuia ulimwengu kuona ukiukaji na jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
PPS imebainisha kuwa waandishi wa habari wanaoshikiliwa katika gereza za kuogofya za Israel wamekabiliwa na vitendo mbalimbali vya unyanyasaji, ikiwemo njaa, kupuuzwa kimatibabu, kuteswa, kutendewa vibaya, unyanyasaji wa kijinsia, na mazingira magumu.
Imeongeza kuwa mamlaka ya Israel imetumia kizuizi cha utawala kuwafunga waandishi wa habari kwa muda usiojulikana bila kufunguliwa mashtaka, mara nyingi ikitumia kile inachokiita “faili za siri,” huku tuhuma za “uchochezi” zikizidi kutumiwa dhidi ya waandishi wa habari kwa sababu ya kuripoti kwao na kutoa maoni.
PPS imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwalinda waandishi wa habari wa Kipalestina na kuhakikisha haki yao ya kufanya kazi, ikisisitiza kuwa vyombo vya habari vimekuwa na jukumu kubwa katika kuweka wazi ukiukaji na jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.
Takwimu hizi za hivi punde zinakuja baada ya vikosi vya Israel kumkamata mwandishi wa habari Mohammed Awad mapema Jumatano wakati wa uvamizi nyumbani kwake huko Beitunia, magharibi mwa Ramallah.