Misri na Imarati zasisitiza kupunguzwa mvutano na kurejeshwa njia ya kidiplomasia kati ya Iran na Marekani
-
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu
Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zimesisitiza umuhimu wa kupunguzwa mvutano na kurejeshwa njia ya mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kkiislamu ya Iran na Marekani.
Sisitizo hilo limetolewa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu katika mazungumzo yao kwa njia ya simu na kujadili uhusiano wa nchi zao mbili pamoja na matukio ya hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Asia Magharibi.
Katika mazungumzo hayo, mawaziri hao wamesisitiza umuhimu wa kuongezwa juhudi za kupunguza mvutano, kurejea kwenye makubaliano ya maelewano kati ya Iran na Marekani, pamoja na kuhakikisha usalama na uhuru wa usafiri wa meli katika maji ya kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Masuala ya Wamisri walio nje ya nchi wa Misri, Badr Abdelatty, na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed Al Nahyan, wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu kuhusu uhusiano wa nchi zao mbili na maendeleo ya hivi karibuni katika eneo hilo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema mazungumzo hayo yalifanyika katika mfumo wa mashauriano na uratibu unaoendelea kati ya nchi hizo mbili kuhusu uhusiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kikanda.
Pande hizo mbili zimesisitiza pia umuhimu wa kurejea katika utekelezaji wa makubaliano ya hati ya maelewano kati ya Marekani na Iran ya Islamabad. Kwa mujibu wa mawaziri hao, hatua hiyo inaweza kufungua njia ya kuanza tena mazungumzo ya kisiasa na kidiplomasia na kuzuia kuenea kwa wigo wa mapigano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati, Abdullah bin Zayed Al Nahyan, pia wameeleza umuhimu wa kuheshimu kanuni za sheria za kimataifa na kulinda usalama, uadilifu na uhuru wa usafiri wa meli katika maji ya kimataifa.
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yao, mawaziri hao wawili walijadili pia matukio na hali ya sasa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.